Gossip

Ruth K Atoa Maneno Mazito Dhidi ya Mulamwah kwa Kutoheshimu Faragha Yake

Ruth K Atoa Maneno Mazito Dhidi ya Mulamwah kwa Kutoheshimu Faragha Yake

Mama wa mtoto wa mchekeshaji maarufu Mulamwah, anayefahamika kwa jina la Ruth K, amezua gumzo mitandaoni baada ya kumtolea uvivu mzazi mwenzake, kufuatia hatua ya msanii huyo kuchapisha picha yake kwenye mitandao ya kijamii bila idhini.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ruth K aliandika ujumbe wa hisia akieleza jinsi alivyojeruhiwa kihisia tangu kuvunjika kwa mahusiano yao takribani miezi mitatu iliyopita. Anasema kuwa ukimya wake umechukuliwa kimakosa kuwa ni udhaifu, na sasa ameamua kusimama kidete kudai heshima yake.

“Mara nyingine kimya huchukuliwa kuwa udhaifu. Haijapita hata miezi mitatu tangu tuachane, lakini tayari nimepitia fedheha na ukosefu wa heshima hadharani – na zaidi kwa faragha,” aliandika Ruth K.

Katika ujumbe huo, Ruth alieleza kuwa anapitia wakati mgumu wa kupona kihisia lakini hali hiyo imekuwa ya kuchosha kutokana na matendo ya dharau kutoka kwa Mulamwah. Alifichua kuwa Mulamwah alimtumia pesa kiasi cha shilingi 5,000 kisha akazirudisha haraka, jambo ambalo alilitaja kuwa ni la dharau. Lakini kilichomuudhi zaidi ni kitendo cha Mulamwah kupakia picha aliyoweka juhudi kubwa kuipiga na kuitayarisha, bila ridhaa yake.

“Unatuma elfu tano halafu unairejesha, kisha unathubutu kuscreenshot picha niliyoitolea jasho? Kiburi ni kikubwa mno,” alisema kwa msisitizo.

Kwa hasira na uchungu, Ruth K alihitimisha ujumbe wake kwa kusema ameamua kuchukua heshima yake tena, akiahidi kuwa ipo siku atasimulia hadithi yake yote kwa umma.

“Siku moja nitaeleza simulizi langu,” aliandika kwa hisia.

Hali hii imezua mjadala mkubwa mitandaoni huku wafuasi wa wawili hao wakigawanyika, wengine wakimuunga mkono Ruth kwa ujasiri wake wa kujieleza, huku wengine wakimtaka aepuke kusambaza mambo ya kifamilia kwenye mitandao ya kijamii.

Hadi kufikia sasa, Mulamwah bado hajatoa kauli rasmi kuhusiana na tuhuma hizo mpya dhidi yake.