Mwanamuziki wa nyimbo za injili kutoka Kenya, Shiru wa GP, amefunguka kuhusu ombi la mwisho la marehemu Betty Bayo, aliyefariki dunia mnamo Novemba 10, 2025, akisema hakutaka kupigwa picha yoyote alipokuwa hospitalini.
Shiru amesema kuwa Betty alimwambia wazi kuwa alikuwa amepambana vya kutosha na kupitia maneno mengi machungu kwenye mitandao ya kijamii, hivyo hakutaka kuwa mjadala tena mtandaoni wakati wa kuugua kwake.
Kwa mujibu wa Shiru, maneno ya Betty yalikuwa ya mwisho kabisa kuhusu taswira yake hadharani, akisema kuwa alimuomba rafiki yake huyo kuhakikisha hakuna mtu anayempiga picha akiwa hospitalini.
Katika kutekeleza hilo, Shiru amesema alilazimika kugombana na baadhi ya watu waliotaka kumpiga picha Betty, jambo ambalo marehemu hakulitaka kufanyika.
Shiru wa GP alikuwa mmoja wa marafiki wa karibu wa Betty Bayo na ndiye aliyekuwa akimuuguza hadi dakika za mwisho za maisha yake.