Afande Selle Awasuta Wasanii Wanaodharau Mashabiki Baada ya Kampeni ya Kususia Kazi Zao
Msanii mkongwe Afande Selle amewakosoa baadhi ya wasanii wa Bongofleva wanaodaiwa kuwadharau mashabiki wao kwa kutoa kauli zinazokera, hasa katika kipindi hiki ambacho Watanzania wameendelea kuendesha kampeni ya kususia kazi za wasanii waliojihusisha na masuala ya ksiasa. Akizungumza kuhusu hali hiyo, msanii huyo amesema kuwa mashabiki ndiyo nguzo muhimu ya mafanikio ya msanii yeyote, hivyo kutoa kauli zinazowaumiza au kuwakejeli ni sawa na kujikatia tawi ulilokalia. Amesisitiza kuwa mafanikio ya wasanii hutokana moja kwa moja na sapoti ya jamii, hivyo ni kosa kubwa kwa msanii kuwabeza mashabiki waliowainua. Msanii huyo mkongwe ameeleza kuwa baadhi ya wasanii wamekuwa wakitoa kauli za kejeli na dharau kufuatia hatua ya wananchi kususia kazi zao, badala ya kujitathmini na kutambua makosa yao. Kwa mujibu wake, hali hiyo imezidi kuchochea hasira za mashabiki na kuongeza mpasuko kati ya wasanii na jamii. Aidha, ametoa wito kwa wasanii wote kutumia kipindi hiki kama funzo, kwa kutuliza kauli zao, kuheshimu maoni ya wananchi na kurejesha mahusiano mema na mashabiki. Ameongeza kuwa kuomba msamaha na kuonyesha unyenyekevu si udhaifu, bali ni ishara ya hekima na ukomavu.
Read More