Mwanamuziki kutoka Kenya, Bahati, amewashangaza mashabiki wake baada ya kufichua kuwa gauni la harusi la mke wake, Diana Marua, litagharimu si chini ya shilingi milioni tano za Kenya.
Kupitia ujumbe wake mtandaoni, amesema kuwa anapanga kufanya harusi ya kifahari ya siku 10 itakayoweka historia barani Afrika, na hatapokea michango yoyote kutoka kwa marafiki au familia kwani atagharamia kila kitu mwenyewe.
Bahati amemtaka Diana kutokuwa na wasiwasi kuhusu suala la kufunga ndoa, akisisitiza kuwa tayari ana mpango maalum wa kufanya sherehe ya kipekee itakayovutia watu wengi.
Msanii huyo amesema kuwa maandalizi ya harusi hiyo yatakuwa makubwa zaidi kuliko ilivyozoeleka, akipanga kufanya siku 10 za sherehe na hafla mbalimbali kabla ya kufikia kilele chake.
Kwa mujibu wa Bahati, siku ya mwisho ya maadhimisho hayo ndiyo itakayokuwa harusi rasmi ya kizungu (white wedding), ambayo anaamini itakuwa ya kukumbukwa na wengi kote Afrika.