Eric Omondi: Polisi Wapuuze Amri ya Risasi
Mchekeshaji maarufu nchini Kenya, Eric Omondi, ameibua mjadala mkali baada ya kutoa wito kwa maafisa wa polisi kupuuza kauli ya Rais William Ruto kuhusu kutumia risasi za miguu dhidi ya watu wanaoharibu biashara za wengine. Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Eric Omondi alisema kuwa polisi ni sehemu ya wananchi na hivyo hawapaswi kuwaadhibu Wakenya wenzao kwa kutumia nguvu kupita kiasi. Akitumia sauti ya ukakamavu, alisisitiza kuwa raia wamechoka na uongozi wa Rais Ruto, hasa kutokana na hali ngumu ya maisha, ukosefu wa ajira, na kupanda kwa gharama ya bidhaa muhimu. “Polisi pia ni Wakenya. Wana familia, wana ndugu. Hii nchi sio ya mtu mmoja, na ni makosa makubwa kutumia risasi kwa wananchi wanaolalamika au kuandamana kwa amani,” alisema Eric Omondi. Kauli ya Eric imekuja siku chache tu baada ya Rais Ruto kunukuliwa akisema kuwa watu watakaohusika na uporaji au uharibifu wa mali wakati wa maandamano wataadhibiwa kwa kupigwa risasi kwenye miguu ili kuzuia uhalifu na kulinda biashara za watu wengine. Lakini kwa upande wake, Eric Omondi amesema kuwa hatua hiyo ni kinyume na haki za binadamu na inachochea ghasia zaidi badala ya kuleta suluhu. Ameitaka serikali kusikiliza kilio cha wananchi badala ya kuwanyamazisha kwa vitisho na nguvu za kijeshi. Tamko hilo limezua hisia mseto mitandaoni na kwenye majukwaa ya kisiasa, huku baadhi ya watu wakimuunga mkono kwa kusema amekuwa sauti ya wanyonge, huku wengine wakimtaka atumie jukwaa lake kwa njia za kujenga badala ya kuikosoa serikali.
Read More