Google Yaianza Maboresho ya Emoji za Android
Google imeanza kufanya maboresho ya muundo wa emoji zinazotumika kwenye simu za Android, hatua inayolenga kuzifanya zifanane kwa kiasi kikubwa na emoji za iPhone zinazotumika kwenye mfumo wa iOS. Mabadiliko hayo yameanza kuonekana katika mfumo mpya wa majaribio wa Android 16, ambapo emoji nyingi zimeboreshwa muonekano wake na kufanana zaidi na zile za Apple. Kwa muda mrefu, emoji za Android zimekuwa na muundo wa kipekee, tofauti na za iOS na Microsoft, kwani Google ilikuwa ikisisitiza kuwa na utambulisho wake binafsi. Kwa ujumla, mfumo wa emoji duniani unaruhusu kampuni kuwa na uhuru wa kubuni muonekano wao, mradi maana ya emoji ibaki ile ile. Hii ndiyo sababu emoji za mifumo mbalimbali zimekuwa na mwonekano tofauti, licha ya kuwasilisha ujumbe unaofanana. Kwa maboresho haya mapya, inatarajiwa kuwa Android na iOS zitakuwa na muundo unaofanana kwa kiwango kikubwa, ingawa tofauti ndogo bado zitabaki, hususan katika rangi za emoji. Asilimia kubwa ya muundo wake itafanana, jambo linalolenga kuboresha mawasiliano ya kidijitali kwa watumiaji. Hatua hii ya Google imezua mijadala mitandaoni, baadhi ya watumiaji wakifurahia mabadiliko hayo kwa urahisi wa mawasiliano, huku wengine wakieleza wasiwasi wa kupotea kwa utofauti wa muundo wa Android. Maboresho haya yanatarajiwa kuonekana rasmi pindi Android 16 itakapotolewa kwa umma.
Read More