KRG The Don Atoa Wito wa Amani Kati ya Kenya na Tanzania Kufuatia Kuzuia kwa Wanaharakati
Msanii na mfanyabiashara maarufu wa Kenya, KRG The Don, ametoa maoni yake kuhusu tukio la wanaharakati wa Kenya waliokamatwa na kuzuiliwa nchini Tanzania hivi karibuni. Akiwa na mtazamo wa kipekee, KRG amesema licha ya wanaharakati hao kudai kuwa walikuwa wakitetea haki, huenda hawakuzingatia mbinu sahihi za kuwasilisha ujumbe wao, jambo ambalo lilichangia wao kujipata matatani. “Ni kweli wanaharakati wana jukumu la kutetea haki, lakini kuna njia sahihi za kufanya hivyo. Kuna uwezekano walihusishwa na ajenda ya kumtetea kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Mbowe, na pengine walilipwa ili kusukuma ajenda hiyo,” alisema KRG. Aidha, KRG alieleza kusikitishwa na mzozo unaoendelea mitandaoni kati ya Wakenya na Watanzania kuhusu suala hilo. Amesisitiza kuwa Kenya na Tanzania ni mataifa ya kindugu, na haipaswi kuwa na mivutano ya kijamii au kisiasa. “Mimi nimekuwa nikisafiri Tanzania mara nyingi, na kila wakati nimepokelewa kwa heshima na mapenzi makubwa. Sioni sababu ya sisi kuchochea chuki kupitia mitandao ya kijamii,” aliongeza. Katika hatua nyingine, KRG amedokeza kuwa anapanga kusafiri hivi karibuni kwenda Tanzania kwa lengo la kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kutafuta muhula mwingine wa uongozi. Kauli ya KRG imepokewa kwa mitazamo tofauti mitandaoni, huku baadhi wakimpongeza kwa msimamo wake wa kuhimiza mshikamano wa Afrika Mashariki, na wengine wakitaka uchunguzi huru kuhusu hali ya wanaharakati waliokamatwa.
Read More