Yvonne Chaka Chaka Akanusha Taarifa Za Kuwahi Kuumia na Kushindwa Kutembea
Mwanamuziki mkongwe kutoka Afrika Kusini, Yvonne Chaka Chaka, ameibuka hadharani kupinga vikali taarifa za uongo zinazosambaa mtandaoni zikidai kuwa aliwahi kusaidiwa kutembea tena na daktari aitwaye Katlego Mothudi baada ya kuanguka na kuumia vibaya. Kupitia mitandao ya kijamii amechapisha makala yaliyokuwa ikizungumzia taarifa hiyo, ambapo amekanusha madai hayo akiyataja kuwa ya kupotosha na yasiyo na ukweli wowote. Amesema hakuna tukio kama hilo lililowahi kutokea na kwamba taarifa hizo zimetungwa kwa lengo la kutangaza bidhaa za makampuni feki kwa kutumia teknolojia ya Akili bandia (AI). Msanii huyo amesema watu wanaosambaza taarifa hizo hawana uadilifu na wako tayari kutumia mbinu zozote, ikiwemo udanganyifu na uongo, kwa ajili ya kujinufaisha kibiashara. Ameongeza kuwa hata daktari anayetajwa katika matangazo hayo ameshtushwa na taarifa hizo kwa kuwa hazina msingi wowote wa kweli. Yvonne ameonya kuwa matumizi mabaya ya teknolojia ya AI pamoja na kuibuka kwa makampuni yasiyoaminika ni tatizo kubwa linalohitaji kuchukuliwa kwa uzito. Amehimiza mashabiki wake na umma kwa ujumla kuwa makini, wachunguze taarifa kabla ya kuziamini au kuzisambaza, na kuepuka kuangukia mitego ya matangazo ya udanganyifu mtandaoni.
Read More