Msanii wa Bongo Fleva kutoka Tanzania, Harmonize, ameendelea kupeperusha vyema bendera ya Afrika Mashariki baada ya kufanya show kali jijini Kampala, Uganda, aliposhiriki kwenye tamasha lililoandaliwa na malkia wa Dancehall kutoka Jamaica, Spice.
Katika show hiyo iliyovutia mashabiki wengi wa muziki wa Dancehall, Harmonize alipanda jukwaani na kuonyesha umahiri wake wa kutumbuiza, akiwasha moto kwa nyimbo zake maarufu zilizowafanya mashabiki kuimba na kucheza kwa furaha.
Ushiriki wake kwenye show ya Spice unaonekana kuwa hatua nyingine muhimu katika kupanua wigo wake wa kimataifa, hasa ukizingatia kuwa tayari ameshirikiana na msanii huyo kupitia wimbo wao wa pamoja “Miss Bantu,” ambao uliwahi kupokelewa vizuri na mashabiki.
Mashabiki waliohudhuria tamasha hilo walionesha mapenzi makubwa kwa Harmonize, wakimtambua kama mmoja wa wasanii wanaoendelea kuiwakilisha vyema Afrika kwenye majukwaa ya kimataifa.