Arsenal imevuka kigingi kigumu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya West Ham United katika dimba la London Stadium.
Katika mtanange uliotawaliwa na upinzani mkali, Leandro Trossard aliibuka shujaa wa ‘Washika Bunduki’ kwa kupachika bao la ushindi dakika ya 83 akimalizia pasi safi ya nahodha Martin Ødegaard. Hata hivyo, ushindi huo haukuja kirahisi, kwani ulihitaji uingiliaji wa teknolojia na uhodari wa kipa kulinda alama tatu.
Mchezo ulifikia kilele cha msisimko pale West Ham walipofunga bao la kusawazisha kupitia kwa Callum Wilson katika dakika za nyongeza. Hata hivyo, mwamuzi alilipeleka tukio hilo kwenye VAR, ambapo ilionekana kuwa kipa wa Arsenal, David Raya,alichezewa rafu kabla ya mpira kuingia wavuni.
Mbali na msaada wa VAR, David Raya alikuwa nyota wa mchezo baada ya kuokoa michomo kadhaa ya hatari (saves), ikiwemo shuti la karibu la Mateus Fernandes, na hivyo kuwahakikishia Arsenal ushindi huo muhimu ugenini.
Matokeo haya yanaiweka Arsenal kileleni mwa msimamo ikiwa na alama tano mbele ya wapinzani wao wakuu, Manchester City, ingawa City wana mchezo mmoja mkononi.
Arsenal sasa inahitaji kushinda mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Burnley na Crystal Palace ili kutangazwa mabingwa wapya. Kwa West Ham, kichapo hiki kinawaacha katika wakati mgumu wakipambana kutoshuka daraja, huku mashabiki wao wakiondoka London Stadium wakiwa na malalamiko dhidi ya maamuzi ya VAR.