Tiktoker kutoka Kenya aitwaye Kabuda ameibua gumzo mitandaoni baada ya kujibu wakosoaji wake kwa kutumia wimbo “Sipangwingwi” wa msanii Exray.
Kabuda, ambaye mara kwa mara hukosolewa kuhusu tabia yake ya kupenda kula chakula kingi, ameamua kujitetea kwa njia ya ubunifu na ucheshi kupitia video aliyochapisha mtandaoni.
Katika video hiyo ambayo imeanza kusambaa kwa kasi, Kabuda anaonekana akivibe na kuimba kwa hisia kipande cha wimbo huo maarufu, akisisitiza kauli kwamba maisha ni yake na hakuna mtu anayepaswa kumwelekeza cha kufanya.
Ujumbe huo umeonekana kama jibu la moja kwa moja kwa watu wanaomshauri kupunguza kula au kubadili tabia zake, huku akionyesha kwamba haungi mkono shinikizo la mitandaoni kuhusu mwonekano au mtindo wa maisha.