
Msanii wa Hip Hop nchini Tanzania, Wakazi, ameibua mjadala mkali mitandaoni baada ya kukosoa vikali aina ya mikataba wanayopewa wasanii wachanga na baadhi ya lebo kubwa za muziki nchini humo. Kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa Instagram, Wakazi alisema kuwa mikataba mingi inalenga kuwanufaisha wamiliki wa lebo huku wasanii wakibaki bila mamlaka ya kazi zao hata zile walizozifadhili kwa pesa zao wenyewe.
Katika maelezo yake, Wakazi alimtaja msanii Harmonize, akifichua kuwa licha ya yeye kugharamia baadhi ya kazi zake binafsi wakati akiwa chini ya lebo ya Wasafi (WCB), bado alilazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha ili aweze kuchukua catalog ya nyimbo alizotoa akiwa na lebo hiyo.
“Kumbuka Harmonize alikuwa anagharamia baadhi ya kazi zake kutoka mfukoni, lakini Wasafi walitaka alipie hela ili achukue catalog yake (wakati wao hata hawaku-invest on),” aliandika Wakazi.
Wakazi aliongeza kuwa hali kama hiyo si ya kipekee, bali ni changamoto ambayo imekuwa ikiwakumba wasanii wengi chipukizi nchini Tanzania. Alisema kuwa kwa kutokuelewa masuala ya kisheria, wengi wao husaini mikataba kwa pupa, hali inayowaacha wakinyonywa kwa muda mrefu bila njia rahisi ya kujinasua.
Wakazi ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wasanii kuhakikisha wanapata ushauri wa kisheria kabla ya kuingia kwenye mikataba, ili kulinda kazi na haki zao. Pia amezitaka lebo za muziki kuwa na uwazi na kuweka mbele maslahi ya wasanii badala ya kutazama faida pekee.
“Muziki ni biashara, lakini isiwe biashara ya kumnyonya msanii aliyetoa jasho lake. Tunahitaji mabadiliko ya kweli kwenye mfumo huu,” alisema.
Kauli hiyo imeungwa mkono na baadhi ya mashabiki na wadau wa sanaa, huku wengine wakitaka kuanzishwe taasisi huru zitakazosaidia wasanii kusoma na kuelewa mikataba kabla ya kuisaini.
Suala la mikataba kandamizi limekuwa likirudiwa mara kwa mara katika mijadala ya burudani nchini Tanzania. Wasanii kama Harmonize, Rayvanny, na wengine waliowahi kujitoa katika lebo kubwa wameelezea wazi namna walivyolazimika kulipa fedha nyingi ili kurejesha uhuru wa kazi zao.