
Tukio la kujeruhiwa kwa msanii mashuhuri wa muziki wa Kenya, Arrow Bwoy, na polisi wakati wa maandamano ya amani limezua taharuki kubwa mitandaoni na kusababisha wasanii wenzake kuibua hisia kali za hasira na kukemea ukatili wa polisi.
Arrow Bwoy alikuwa ameungana na rapa maarufu Khaligraph Jones pamoja na raia wengine katika maandamano ya kupinga ukatili wa vyombo vya usalama. Hata hivyo, maandamano hayo yaliishia kwa vurugu baada ya polisi kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu ya machozi na nguvu kupita kiasi, hali iliyomwacha Arrow Bwoy amejeruhiwa.
Khaligraph Jones alilalamikia tukio hilo kupitia mitandao ya kijamii, akisema kwa uchungu kuwa waandamanaji walikuwa wakifanya maandamano kwa amani, lakini walishambuliwa na polisi waliokuwa wakifyatua mabomu ya machozi moja kwa moja kwao. Alisema kitendo hicho ni mfano tosha wa ukatili wa polisi unaopaswa kukomeshwa mara moja.
“Unapofanya maandamano ya amani halafu wanaanza kukupiga risasi za mabomu ya machozi… Kukomesha ukatili wa polisi nchini Kenya ni muhimu sana. #RespectTheOGs,” Alielezea kwa uchungu Khaligraph Jones, ambaye alikuwa sambamba na Arrow Bwoy wakati wa maandamano hayo.
Naye mchumba wa Arrow Bwoy na mama wa mtoto wake, Nadia Mukami, alionekana kuguswa sana na tukio hilo. Kupitia ujumbe alioutuma mtandaoni, aliandika kwa hasira kuwa polisi hawapaswi kumshika baba wa mtoto wake na kutaka ukatili huo ukome mara moja.
“Nyinyi mafala msimguse baba watoto wangu!!!! #EndPoliceBrutality Nimejam ata!!!!!,” Aliandika kwa hasira Instagram.
Kauli za wasanii hao zimeungwa mkono na maelfu ya mashabiki na wakenya wa kawaida, huku wengi wakitumia mitandao ya kijamii kulaani hatua ya polisi kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji wa amani. Hashtag kama #EndPoliceBrutality na #RespectTheOGs zimeendelea kutrendi huku wito ukitolewa kwa serikali kuwajibisha maafisa waliohusika.
Tukio hili limezua mjadala mpana kuhusu haki ya kuandamana na uhuru wa kujieleza nchini Kenya, huku wasanii wakionyesha kuwa wako tayari kusimama na wananchi kupigania haki na mabadiliko katika jamii.