
Baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 15, hatimaye kampuni ya Meta imezindua rasmi toleo la WhatsApp kwa iPad. Kwa muda mrefu, watumiaji wa iPad walikosa njia ya moja kwa moja kutumia WhatsApp, tofauti na watumiaji wa simu na kompyuta ambao walikuwa na app kamili au toleo la WhatsApp Web.
Kwa mujibu wa taarifa ya WhatsApp wiki hii, toleo la iPad sasa linapatikana kupitia App Store na linatumia mfumo wa multi-device linking. Watumiaji wanaweza kuunganisha iPad yao na akaunti ya WhatsApp kutoka kwenye simu kwa kuskani QR code, hivyo kuwezesha kusoma na kutuma ujumbe, picha, video, na hata kupiga simu za sauti na video bila hitaji la kuweka laini ya simu kwenye iPad.
Uzinduzi huu ni hatua muhimu kwa Meta, kwani washindani kama Telegram na Signal tayari walikuwa na matoleo ya iPad. WhatsApp sasa inapanua wigo wake wa matumizi, na hatua hii inatarajiwa kuongeza idadi ya watumiaji, hasa miongoni mwa waliokuwa wakitegemea njia zisizo rasmi kutumia huduma hiyo kwenye iPad.