Entertainment

Hanstone Aibua Madai Mazito Dhidi ya WCB Wasafi

Hanstone Aibua Madai Mazito Dhidi ya WCB Wasafi

Msanii wa Bongo Fleva, Hanstone, amevunja ukimya kuhusu maisha yake ndani ya lebo ya WCB Wasafi, akieleza hadharani changamoto alizokumbana nazo kipindi alichokuwa akihudumu humo.

Akizungumza juzi kwenye mahojiano, Hanstone alidai kuwa alikaa ndani ya WCB kwa kipindi cha miaka mitatu bila kutambulishwa rasmi kama msanii wa lebo hiyo. Katika kipindi hicho, alieleza kuwa alihusika katika kuandika nyimbo kwa wasanii wengine, wakiwemo majina makubwa kama Diamond Platnumz, lakini hakuwahi kulipwa chochote kwa kazi hiyo.

 “Nilitumika kuandika nyimbo kwa wasanii waliokuwa juu, lakini sikuwahi kupewa nafasi yangu wala stahiki zangu. Niliamini kwenye mchakato, lakini haikuwa kama nilivyotarajia,” alisema Hanstone kwa hisia.

Kwa muda mrefu, mashabiki na wadau wa muziki wamekuwa wakimtaja Hanstone kama msanii asiye na subira, sifa ambayo imeonekana kuwa chanzo cha yeye kutopata nafasi ya kung’aa akiwa chini ya lebo hiyo ya WCB. Hata hivyo, msanii huyo amekana madai hayo, akisema alijitahidi kuwa mvumilivu, lakini hakupata fursa aliyostahili.

Kauli ya Hanstone imezua mjadala mkubwa mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakionesha huruma na kumuunga mkono, wakati wengine wakihimiza wasanii chipukizi kuwa na uvumilivu zaidi wanapojiunga na lebo kubwa kama WCB.

Kwa sasa, bado haijajulikana ikiwa Hanstone atachukua hatua za kisheria au ataendelea na muziki kama msanii huru nje ya lebo hiyo. Mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona hatua yake inayofuata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *