Instagram imezindua mfumo mpya wa algorithm unaowawezesha watumiaji kudhibiti maudhui wanayoona kwenye ukurasa wao wa nyumbani. Mfumo huu mpya unalenga kubinafsisha uzoefu wa kila mtumiaji kulingana na maslahi yake binafsi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Instagram, sasa watumiaji wanaweza kuunda algorithm zao wenyewe. Hii inamaanisha unaweza kuamua ni aina gani ya posts unazopendelea kuona ama ni michezo, filamu, comedy, masomo, sayansi, au mada maalum unayopenda.
Mfumo mpya wa akili bandia (AI) wa Instagram utachambua posts zinazofanana na maudhui uliyoyachagua, kuhakikisha kwamba unapata zaidi ya kile unachokipenda. Kwa mfano, kama ukichagua filamu za aina ya comedy, algorithm itakuonyesha posts nyingi zinazohusiana na filamu hizo, ikiongeza uwezekano wa kupata taarifa na burudani zinazokidhi ladha yako.
Watumiaji wanasema mfumo huu ni hatua muhimu katika kuboresha uzoefu wa mtumiaji, kwani sasa hakuna haja ya kupoteza muda kuangalia maudhui yasiyokufaa. Pia unatoa uhuru mkubwa kwa kila mtu kuunda feed yake ipasavyo.
Instagram imesema mfumo huu mpya unaanza hatua kwa hatua na utazinduliwa rasmi kwa watumiaji wote ndani ya wiki chache zijazo.