Msanii wa muziki wa injili, Bella Kombo, ameweka bayana msimamo wake kufuatia shinikizo kutoka kwa baadhi ya mashabiki waliomtaka afute tattoo alizonazo mwilini.
Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni, Bella amesema yuko tayari kupokea maoni ya watu, lakini hatokubali kuhatarisha afya wala maisha yake kwa lengo la kuwafurahisha wengine. Ameeleza kuwa tattoo hizo zina maana kubwa kwake, kwani ni sehemu ya historia na safari ya maisha yake, na zitabaki mwilini mwake kama ushuhuda wa yale aliyopitia.
Msanii huyo amesisitiza kuwa kumtumikia Mungu hakupimwi kwa muonekano wa nje, bali kwa moyo wa mtu, matendo yake na ujumbe anaowafikishia watu kupitia huduma yake ya muziki.
Bella Kombo amesema ataendelea kumtumikia Mungu kwa kipaji chake na kueneza ujumbe wa matumaini kupitia muziki wake, bila kuyumbishwa na shinikizo au lawama kutoka watu.
Kauli ya Bella imezua mjadala mkubwa mitandaoni, ambapo baadhi ya wadau wakidai kuwa kama mwimbaji wa injili, anapaswa kuendana na matarajio ya jamii. Hata hivyo, kundi kubwa la mashabiki limemuunga mkono, likisisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kufanya maamuzi juu ya mwili wake bila kulazimishwa.