AT Amvua Master J Hadhi ya Prodyuza: “Si Mzalishaji Bali Ni Mmiliki wa Studio”
Msanii wa Bongefleva AT ameibua mjadala mkali katika tasnia ya muziki wa Tanzania baada ya kutoa kauli nzito zinazomvua hadhi Master J kama prodyuza halisi. Kwa mujibu wa AT, Master J si mzalishaji wa muziki bali ni mmiliki wa studio maarufu za MJ Records. Amefafanua kuwa kitaaluma, Master J alisomea masuala ya electronics na sio music production, hivyo uwezo wake unajikita zaidi kwenye upande wa vifaa na ufundi kuliko uandaaji wa muziki. AT ameeleza kuwa ingawa Master J amekuwa na mchango mkubwa kwa sababu ya kumiliki studio na kutoa nafasi kwa wasanii kurekodi, hana ujuzi wa kitaaluma wa kumwezesha kuhesabiwa miongoni mwa maprodyuza wakubwa waliounda historia ya muziki wa Bongofleva. Aidha, AT amefichua kuwa katika moja ya warsha za muziki zilizofanyika nchini Afrika Kusini, Master J aliwahi kushindwa kabisa kuchangia hoja zozote muhimu kuhusiana na studio na uzalishaji muziki, jambo lililomfanya ashuke hadhi mbele ya wenzake. Hata hivyo amempa changamoto Master J kuthibitisha nafasi yake kama prodyuza halisi kwa kuonyesha albamu ambazo amewahi kuzitengeneza yeye mwenyewe kuanzia hatua ya mwanzo hadi mwisho. Kauli ya AT imekuja mara baada ya msanii mkongwe Juma Nature kunukuliwa katika moja ya mahojiano akidai hajawahi kumkubali Master Jay kama producer. Nature alieleza kuwa kipindi cha nyuma Master Jay alitamani kuwa kama P Funk Majani, hali iliyomfanya baba yake mzazi kumnunulia vyombo vya muziki na si kwa ubunifu au kipaji chake binafsi.
Read More