Bobi Wine Aonya Wasanii Kuhusu Maudhui ya Nyimbo Zao

Bobi Wine Aonya Wasanii Kuhusu Maudhui ya Nyimbo Zao

Msanii nguli wa muziki na mwanasiasa kutoka Uganda, Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine, ameonya wasanii wa kizazi kipya kwamba mashairi yasiyo na maadili na yanayokosa maudhui yenye maana huenda yakaathiri urithi wao wa muziki. Bobi Wine, ambaye ana historia ndefu kwenye tasnia ya burudani kabla ya kuingia kwenye siasa, amesema muziki una nafasi kubwa ya kubadilisha jamii na kumbaki kama urithi wa kudumu. Kwa mujibu wake, kazi za sanaa ambazo zinajikita kwenye matusi, udhalilishaji na ujumbe usio na maadili mara nyingi huishia kusahaulika, huku muziki wenye thamani ya kijamii ukibaki kwa vizazi vingi. Mwanasiasa huyo ameeleza kwamba yeye binafsi anajivunia kutumia muziki wake kama chombo cha kuhamasisha jamii na kupigania haki, jambo ambalo limemsaidia kuendelea kukumbukwa kwa miaka mingi. Alisisitiza kuwa vijana wengi wanapenda burudani, lakini ni jukumu la wasanii kuhakikisha muziki wao unachangia kuelimisha na kuboresha jamii badala ya kuathiri vibaya maadili. Bobi Wine amewataka wasanii wa Afrika Mashariki na bara kwa ujumla kuzingatia athari za muziki wao katika maisha ya watu na kufikiria ni urithi upi wanataka kuacha. Kwa sasa, licha ya changamoto za kisiasa na shinikizo analokabiliana nalo nchini Uganda, Bobi Wine anaendelea kutumia jukwaa la muziki na siasa kushinikiza mabadiliko ya kijamii na kisiasa.

Read More
 Nyota Ndogo Atoa Onyo kwa Wasichana wa Ughaibuni

Nyota Ndogo Atoa Onyo kwa Wasichana wa Ughaibuni

Msanii Nyota Ndogo ametoa ujumbe mzito kwa wasichana wa Kiafrika wanaofanya kazi katika mataifa ya Kiarabu, akiwataka kuwa waangalifu na mahusiano ya mtandaoni. Kupitia Instgram yake, ameeleza kuwa mabinti wengi hujikuta wakitumika kihisia na kifedha na wanaume wasiowajali, huku wakiteseka kazini kwa masharti magumu. Nyota Ndogo amesema kuwa baadhi ya wanaume huwatumia wanawake walioko nje ya nchi kama chanzo cha fedha, wakiwadanganya kwa maneno matamu ya mapenzi. Amesema wapo wanaume wanaowalazimisha wanawake kuwatumia pesa za kodi, miradi au matumizi ya kila siku, huku wao wakifaidika kwa urahisi bila kuchangia chochote. Akiwa na uzoefu binafsi wa kufanya kazi ya ndani akiwa na umri wa miaka 17, Nyota amesema anafahamu vyema uchungu wa maisha ya ughaibuni. Alisisitiza kuwa wanawake wengi hujikuta wakibeba mzigo mara mbili kazi ngumu na mahusiano yenye mateso ya kihisia. Hitmaker huyo wa Watu na Viatu, ameonya kuwa tabia hii imewafanya baadhi ya wanaume kuwa wavivu wa maisha, kwa sababu wanategemea msaada kutoka kwa wanawake walioko nje. Alishauri mabinti wajifunze kujipenda na kutosema kila kitu mtandaoni, kwani baadhi ya watu hutumia taarifa hizo kuwadhulumu. Nyota Ndogo amemalizia kwa kuwaombea wasichana walioko ughaibuni, akisisitiza kuwa wanahitaji ulinzi wa Mungu dhidi ya udanganyifu wa mapenzi na hali ngumu za kazi. Kauli yake imeibua hisia mbalimbali mitandaoni, wengi wakikiri kuguswa na ujumbe huo wa uhalisia.

Read More
 Morocco Yaizamisha Madagascar 3-2, Yatwaa Ubingwa wa CHAN

Morocco Yaizamisha Madagascar 3-2, Yatwaa Ubingwa wa CHAN

Timu ya taifa ya Morocco (Atlas Lions) imeandika historia tena katika anga la soka barani Afrika baada ya kutwaa taji lake la tatu la Mashindano ya Soka kwa Wachezaji wa Ndani ya Afrika (CHAN), kwa kuichapa Madagascar kwa mabao 3-2 katika fainali ya kusisimua iliyopigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani, Nairobi. Morocco, ambao waliwahi kutwaa taji hili mwaka 2018 na 2020, walionyesha kiwango cha juu licha ya upinzani mkali kutoka kwa Madagascar waliocheza kwa ari kubwa wakitafuta taji lao la kwanza. Nyota wa mchezo huo alikuwa mshambulizi mahiri Oussama Lamlaoui, ambaye alitikisa nyavu mara mbili, ikiwa ni pamoja na bao maridadi alilofunga kutoka umbali wa yadi 40. Bao hilo la kipekee liliibua shangwe uwanjani na kumfanya kumaliza mashindano akiwa mfungaji bora kwa jumla ya mabao sita. Ushindi huo haukuwa tu fahari kwa Morocco bali pia ulijumuisha zawadi nono ya pesa taslimu, shilingi milioni 453, ilhali washindi wa pili, Madagascar, waliyoonyesha kandanda safi, waliondoka na kitita cha shilingi milioni 155. Fainali hiyo ya kuvutia ilihudhuriwa na viongozi wa juu wa soka na serikali, akiwemo Rais wa Kenya William Ruto, Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) Gianni Infantino, na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe. Uwepo wao uliongeza hadhi ya tukio hilo na kudhihirisha maendeleo ya soka barani Afrika.

Read More
 Jackie Matubia: Sihusiki na Sakata la Ellah na Odek

Jackie Matubia: Sihusiki na Sakata la Ellah na Odek

Mwigizaji na mama wa watoto wawili, Jackie Matubia, amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya jina lake kuhusishwa na drama ya kifamilia inayomkumba Ellah Ray, dada yake sosholaiti Amber Ray, na aliyekuwa mchumba wake Steve Odek. Matubia, amesema hana uhusiano wowote na sakata hilo na ameonya watu wanaomchafulia jina kutumia uvumi mitandaoni. Kupitia Insta Story yake, alikanusha madai hayo akieleza kuwa amechoshwa na tabia ya watu kutumia akaunti feki kumhusisha na kashfa ambazo hazina msingi. Mrembo hyo alisisitiza kuwa, iwapo watu wanataka kumuhusisha na mambo ya uhusiano, basi angalau wawe na ushahidi wa kweli, kwani kwa sasa wanamtupia lawama zisizomhusu. Kauli yake imeweka bayana msimamo wake wa kutoshirikiana na sakata hilo na kutaka jina lake libaki safi. Jackie alilazimika kujibu baada ya Ellah Ray kumuanika Steve Odek kwa usaliti na kudai anahusiana na wanawake kadhaa, jina la Matubia likiwemo katika tetesi hizo.

Read More
 Ellah Aachana Rasmi na Mzazi Mwenzake Steve Odek

Ellah Aachana Rasmi na Mzazi Mwenzake Steve Odek

Ellah Ray, dada yake sosholaiti maarufu Amber Ray, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kutangaza kuvunja uhusiano wake na baba wa mtoto wake, Steve Odek, huku akimshtumu kwa usaliti na mahusiano ya siri na wanawake kadhaa jijini Nairobi, akiwemo mwigizaji Jackie Matubia. Kupitia mfululizo wa jumbe za hisia kwenye Insta Story, Ellah alisema hatimaye amefikia kikomo baada ya kuvumilia zaidi ya miaka mitatu ya kile alichokiita kudhalilishwa, kutopewa heshima na usaliti wa mara kwa mara. Alifichua kuwa kwa muda mrefu alijikuta akibeba maumivu kimya kimya na kuendelea kusimama na Odek licha ya onyo nyingi alizopewa. Ellah aliongeza kuwa anajutia hatua yake ya kumtetea mpenzi wake wa zamani, hali iliyomfanya hata kupoteza uhusiano mzuri na baadhi ya wanafamilia wake kwa sababu ya kumlinda. Kufuatia madai hayo, mitandao ya kijamii imewaka moto huku mashabiki wakitoa maoni tofauti, wengine wakimuunga mkono kwa ujasiri wake wa kusema ukweli, na wengine wakisubiri majibu ya wale waliotajwa kwenye sakata hilo.

Read More
 Mfumo wa Android Umeanzisha Mwonekano Mpya wa Call-Screen

Mfumo wa Android Umeanzisha Mwonekano Mpya wa Call-Screen

Mfumo wa uendeshaji wa Android umeleta mabadiliko ya kuvutia katika sehemu ya call-screen, sehemu inayowaonesha watumiaji picha na taarifa wakati mtu anapopigia simu. Mabadiliko haya yanajumuisha mfumo mpya unaoitwa “Calling Card”, ambao umeboresha kabisa uzoefu wa kupokea simu. Kwa mfumo huu mpya wa Calling Card, picha ya mpigia simu sasa inaonekana kwa ukubwa wa skrini nzima (full screen) na kwa mtindo wa kisasa zaidi unaowezesha mtumiaji kuchagua ni picha gani anayotaka ionekane pale anapopigiwa simu. Zaidi ya hayo, mtumiaji anaweza kubadilisha maandishi yanayohusiana na jina la mpigia simu pamoja na rangi za maandishi hayo, hivyo kufanya mwonekano kuwa wa kipekee na wa kibinafsi. Mabadiliko haya yanatoa uhuru zaidi kwa watumiaji wa Android kuunda uzoefu wa simu unaoendana na ladha zao na mitindo wanayopendelea, na kuifanya sehemu ya kupokea simu kuwa ya kuvutia zaidi na rahisi kutumia. Kwa sasa, mabadiliko haya yameanza kuletwa kwa baadhi ya watumiaji na yanatarajiwa kufikia simu nyingi zinazotumia mfumo wa Android kwa hatua kwa hatua katika siku zijazo.

Read More
 Mabingwa Watetezi Senegal Wanyakuwa Nafasi ya Tatu CHAN 2024

Mabingwa Watetezi Senegal Wanyakuwa Nafasi ya Tatu CHAN 2024

Senegal imefanikiwa kunyakua nafasi ya tatu kwenye michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 baada ya kuichapa Sudan kwa mikwaju ya penalti 4-2, kufuatia sare ya bao 1-1 katika dakika za kawaida na nyongeza, jana jioni. Mabingwa watetezi hao walionekana kuonyesha ustadi na uthabiti mkubwa katika mechi hiyo ya kutafuta nafasi ya tatu, hasa baada ya kukataliwa fursa ya kucheza fainali baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti na Morocco katika nusu fainali. Sudan, ingawa ilionyesha mapambano makali na kuonesha kasi ya ushindani, haikuweza kufanikisha ndoto ya kuibuka na medali ya tatu kwenye mashindano haya ya CHAN. Hata hivyo, harakati zao zilitambulika kama mojawapo ya matukio mazuri katika michuano hii. Michuano ya CHAN 2024 itakamilika leo katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi, ambapo mabingwa mara mbili Morocco watakutana na timu mpya kwenye fainali, Madagascar, ambayo imefuzu kwa mara ya kwanza kufikia hatua hiyo.

Read More
 John Blaq: Akaunti Yangu ya YouTube Ilichukuliwa kwa Mabavu na Black Market

John Blaq: Akaunti Yangu ya YouTube Ilichukuliwa kwa Mabavu na Black Market

Staa wa muziki kutoka Uganda, John Blaq, amefunguka kuhusu sababu iliyopelekea mashabiki wengi kudhani kuwa aliacha muziki kwa muda. Amedai kuwa hali hiyo ilitokana na mgogoro ulioibuka kati yake na uongozi wa lebo ya Black Market kipindi cha janga la COVID-19. Kwa mujibu wa msanii huyo, tofauti hizo zilifikia hatua ya kumpokonya akaunti yake ya YouTube ambayo ilikuwa imejikusanyia zaidi ya wafuasi 100,000. Alifafanua kuwa uongozi wa lebo hiyo ulimtaka alipe kiasi cha shilingi milioni 150 ili kurejeshewa akaunti hiyo, jambo ambalo hakuweza kulitekeleza kutokana na changamoto za kifedha wakati huo. John Blaq alisema kutokana na hali hiyo alilazimika kuanzisha kituo kipya cha YouTube, hatua iliyowafanya mashabiki wake wengi kudhani kuwa alikuwa ameweka kando muziki. Pia alibainisha kwamba hakuwahi kusaini mkataba rasmi na Black Market, bali walishirikiana kama ndugu katika kazi. Hata alipojaribu kutafuta maridhiano, juhudi zake hazikufanikiwa baada ya upande huo kukataa suluhu. Licha ya changamoto hizo, John Blaq amesema hakuwahi kufikiria kuacha muziki. Kwa sasa anafanya vizuri na albamu yake mpya African Buoy yenye jumla ya nyimbo 15, ambapo amewashirikisha wasanii kama Maro, Skales, Laika na wengine wengi. Albamu hiyo imepokelewa vizuri na mashabiki, ikionesha kuwa msanii huyo bado anaendelea kuimarisha nafasi yake katika muziki wa Afrika Mashariki.

Read More
 Zuchu Afunguka Kuhusu Madai ya Kubeza Wasanii wa Kenya Kablaya Fainali za CHAN

Zuchu Afunguka Kuhusu Madai ya Kubeza Wasanii wa Kenya Kablaya Fainali za CHAN

Msanii wa muziki kutoka Tanzania, Zuchu, amekanusha taarifa zilizokuwa zikisambaa mitandaoni zikidai kwamba hatoshirikiana na wasanii wa Kenya kwa sababu ya madai ya Wakenya kumtusi Rais Samia Suluhu Hassan. Katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Kiss 100, Zuchu ameeleza kuwa hajawahi kutoa kauli hiyo na kusisitiza kuwa habari hizo hazina ukweli wowote. Amesema kuwa taarifa hizo zilitungwa kwa lengo la kumharibia jina na kumkosanisha na mashabiki wake wa Kenya. Zuchu ameweka wazi kuwa hana nia yoyote mbaya kwa wasanii wa Kenya, bali anawaheshimu kwa vipaji vyao. Ameeleza pia kuwa tayari ameshirikiana nao kwenye miradi yake ya muziki, wakiwemo wasanii wa kundi la Hart the Band, waliopata nafasi kwenye albamu yake. Taarifa hizo ziliibuka muda mfupi baada ya Zuchu kuwasili Kenya kwa ajili ya kutumbuiza leo kwenye fainali za CHAN 2024 katika uwanja wa Kasarani, ambapo atashiriki jukwaa moja na wasanii wengine wakubwa akiwemo Savara na Eddy Kenzo. Kauli yake sasa imeweka wazi msimamo wake na kumaliza tetesi zilizokuwa zikisababisha mjadala mkali mitandaoni kuhusu mahusiano ya muziki kati ya Tanzania na Kenya, akisisitiza mshikamano na ushirikiano wa kisanaa badala ya mgawanyiko. Baadhi ya wadau wa michezo na mashabiki wamehoji iwapo pesa hizo zitatolewa, huku wengine wakisisitiza kuwa wasanii wanapaswa kuwa makini na ahadi wanazotoa kwa umma ili kuepusha migongano na kuharibu taswira ya michezo nchini.

Read More
 Mariga: Bahati Anatafuta Kiki, Sio Kusaidia Harambee Stars

Mariga: Bahati Anatafuta Kiki, Sio Kusaidia Harambee Stars

Naibu Rais wa Shirikisho la Soka Nchini Kenya (FKF), McDonald Mariga, ameibua maswali kuhusu ahadi ya msanii Bahati ya kutoa KSh 1 milioni kwa wachezaji wa Harambee Stars. Kwenye mahojiano na SPM Buzz, Mariga amesema licha ya Bahati kutangaza hadharani mchango huo, hajawahi kuwasilisha fedha hizo kwa wachezaji kama alivyoahidi. Ameeleza pia kutoridhishwa na tabia ya msanii huyo kuanika ahadi kubwa mitandaoni bila utekelezaji, akisisitiza kuwa kitendo hicho kinaashiria zaidi kutafuta umaarufu badala ya kusaidia timu. Hali hii inajiri baada ya Bahati kudai kwamba Mariga anahujumu mchakato wa kuzikabidhi pesa hizo kwa wachezaji wa Harambee Stars kwa kutochukua simu zake. Mariga, kwa upande wake, anashikilia kuwa msanii huyo hana nia ya dhati ya kutimiza ahadi hiyo, na kwamba hatua yake ni ya kujitafutia kiki. Ahadi hiyo ya Bahati ilitolewa wiki kadhaa iliyopita baada ya Harambee Stars kushinda mechi muhimu, ambapo alitangaza kuwa angechangia kiasi hicho kama motisha kwa wachezaji. Hata hivyo, kauli zinazokinzana kati ya pande hizi mbili sasa zimezua sintofahamu na mjadala mkali miongoni mwa mashabiki.

Read More
 Willy Paul Akosoa Waandaaji wa CHAN kwa Kupuuza Wasanii wa Kenya

Willy Paul Akosoa Waandaaji wa CHAN kwa Kupuuza Wasanii wa Kenya

Msanii wa Kenya, Willy Paul, ameibua maswali kuhusu uteuzi wa wasanii waliopangwa kutumbuiza katika fainali ya Mashindano ya CHAN 2024 yatakayofanyika leo Jumamosi katika uwanja wa Kasarani ambapo Morocco itachuana na Madagascar. Kupitia Instastory,Willy Paul ameonekana kutoridhishwa na uteuzi huo, akidokeza kuwa waandaaji huenda walipuuzia nafasi ya kuhusisha wasanii wengine wa Kenya ambao wangeweza kupeperusha bendera ya taifa ipasavyo kwenye tukio hilo kubwa. Kauli ya Willy Paul sasa imechochea mjadala mitandaoni kuhusu nafasi ya wasanii wa Kenya katika matukio ya kimataifa, huku baadhi ya mashabiki wakihisi kuwa nchi inapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi kupitia muziki wake kwenye majukwaa ya aina hii. Hayo yote yaliibuka muda mfupi baada ya waandaaji wa mashindano hayo kutangaza kuwa Savara wa Sauti Sol, nyota wa Tanzania Zuchu, na mshindi wa tuzo za kimataifa kutoka Uganda Eddy Kenzo, sio tu watatumbuiza siku ya fainali, bali pia wameandaa na kuimba anthem rasmi ya CHAN 2024.

Read More
 Brown Mauzo Akiri Bado Ana Hisia kwa Vera Sidika

Brown Mauzo Akiri Bado Ana Hisia kwa Vera Sidika

Penzi la Vera Sidika linaonekana kuendelea kumtesa msanii wa muziki Brown Mauzo, hii ni baada ya kukiri hadharani kwamba bado anampenda sosholaiti huyo licha ya kutengana kwao miezi kadhaa iliyopita. Mauzo amefunguka kupitia majibu kwa shabiki mmoja aliyemwandikia mtandaoni akisema walipendeza sana akiwa na Vera. Katika jibu lake, msanii huyo alikubali kuwa bado moyo wake haujamtoa Vera na kwamba anatamani kama wangeweza kurudiana. Kwa mujibu wa Mauzo, uhusiano wake na Vera haukuwa wa kawaida kwani ulimjengea familia na kumpa mtoto, jambo analolitaja kama kumbukumbu na baraka kubwa katika maisha yake. Ameeleza kwamba Vera ataendelea kubaki mtu wa kipekee moyoni mwake kwa sababu ya nafasi aliyopewa katika maisha yake. Uhusiano wa wawili hao uliwahi kuwa gumzo kubwa mitandaoni, uliojaa matukio ya kifahari, safari za kifamilia na hadithi za kimapenzi zilizoshirikishwa kwa mashabiki. Hata hivyo, baadaye walitangaza kuachana, kila mmoja akichukua mwelekeo tofauti. Vera alirudi kujikita katika biashara na maisha ya mitindo, huku Mauzo akijitahidi kurejea kwa nguvu kwenye muziki. Kauli yake ya sasa imeibua hisia mseto mitandaoni, baadhi ya mashabiki wakimtia moyo kutafuta njia ya kusuluhisha tofauti zao na kumrudisha Vera, huku wengine wakimtaka akubaliane na hali na kuendelea mbele bila kumshikilia penzi la zamani.

Read More