Mzozo mkali wa maneno umeibuka tena kwenye mitandao ya kijamii kati ya wasanii wa muziki wa Bongo Fleva, Nay wa Mitego, Billnass na mkewe Nandy, ukihusisha tuhuma za fitna, chuki na wivu wa maendeleo. Chanzo cha mvutano huo ni kauli ya Billnass aliyodai kuwa alipitia fitna za kutaka kufungwa kwa kesi ya wizi ambayo Nay wa Mitego alihusishwa nayo kwa kauli zisizo rasmi. Billnass, kupitia mahojiano yake na East Africa Radio, alionesha wazi kutoridhishwa na kile alichokiita hila zilizopangwa dhidi yake na watu aliowahi kuwachukulia marafiki. Baada ya maneno hayo, Nay wa Mitego hakusita kujibu kupitia sehemu ya maoni kwenye posti hiyo. Nay alimtaja Billnass kuwa ni msanii mjinga anayependa kiki bila mipaka na kumuita mwizi ambaye alistahili hata kifungo kwa tabia zake. “Acha nikupe unachotaka, wewe ni mwizi, ungeenda jela kwa tabia yako ya wizi. Nina kazi nyingi za kufanya, siwezi kushughulika na kukukandamiza wewe. Mgande Nandy ivyo ivyo ili usije ukaendelea na udokozi,” aliandika Nay wa Mitego. Kauli hiyo iliwasha moto zaidi pale mke wa Billnass, msanii Nandy, alipoamua kumjibu Nay moja kwa moja kwa hasira kali. Kupitia sehemu ya maoni, Nandy alimshutumu Nay kwa wivu na kumuita mvuta bangi, huku akidai kuwa ana chuki kutokana na kushindwa kimaisha. “Nay wa Mitego wewe cho…k…o, jina langu limeingiaje hapo? Mvuta bangi wewe! Una wivu wa maendeleo. Umejaribu kupambana umeshindwa, umebaki kuwa shabiki. Wa kuibiwa muibiwe nyie, na mnacho cha kuibiwa kwanza? Endelea na chaka zako ujikomboe, maisha upande huu mzito boob utasanda! Kithetheeee wewe, fyuu,” aliandika Nandy kwa hasira. Mashabiki kwenye mitandao wamegawanyika, baadhi wakimtetea Nay kwa kusema anasema ukweli bila uoga, huku wengine wakimtaka apunguze maneno ya matusi na wivu. Wengine wamewaomba wasanii hao warekebishe tofauti zao kwa hekima na busara badala ya kurushiana maneno hadharani. Kwa sasa, hakuna dalili za pande hizi kupoa, na mashabiki wanaendelea kufuatilia kwa karibu kuona ni nani atarushia dongo linalofuata.
Read More