Lizer Classic Amkataa S2kizzy, Asema Hana Historia ya Kuwatoa Wasanii

Lizer Classic Amkataa S2kizzy, Asema Hana Historia ya Kuwatoa Wasanii

Prodyuza wa muziki kutoka Tanzania, Lizer Classic, ameibua mjadala baada ya kumkataa S2kizzy kama prodyuza bora wa muziki wa Bongo Fleva. Lizer amesema kuwa licha ya S2kizzy kujinadi sana kuwa ndiye kinara wa utayarishaji wa muziki kwa sasa, hana historia ya kuwatoa wasanii wapya kwenye tasnia. Kwa mujibu wa Lizer, ukubwa wa prodyuza hupimwa si tu kwa hits anazotengeneza, bali pia kwa mchango wake katika kukuza na kulea vipaji vipya. Ametolea mfano Master Jay na P Funk Majani, ambao amewapongeza kwa kuwa nguzo kubwa za muziki wa Bongo Fleva kutokana na lebo zao zilizozalisha wasanii wengi waliokuja kuwa majina makubwa. Kauli ya Lizer imezua mjadala mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakimtetea S2kizzy kwa ubunifu na kazi kubwa alizofanya, ilhali wengine wakikubaliana na mtazamo wa Lizer kwamba mchango wa kudumu kwenye tasnia hupimwa zaidi kwa kizazi unachoibua.

Read More
 Cindy Sanyu Kutetea Wanamuziki wa Upinzani kwa Rais Museveni

Cindy Sanyu Kutetea Wanamuziki wa Upinzani kwa Rais Museveni

Rais wa Chama cha Wanamuziki Uganda (UMA), Cindy Sanyu, ametangaza mpango wa kuwasilisha rasmi malalamiko kwa Rais Yoweri Museveni kuhusu changamoto zinazowakumba wanamuziki wanaoamua pia kujihusisha na siasa za upinzani. Cindy amesema kuwa serikali mara nyingi imekuwa ikidhoofisha taaluma ya wasanii wanaoingia katika ulingo wa kisiasa, jambo analoliona kama kikwazo kwa maendeleo ya tasnia ya muziki nchini humo. Kwa mujibu wa mwanamuziki huyo, suala hilo atalibua katika kikao kijacho ambacho viongozi wa UMA wanatarajia kufanya na Rais Museveni. Amesisitiza kuwa hoja yake kuu itakuwa ni kutaka kuwepo na utofauti kati ya taaluma ya muziki na ile ya kisiasa, ili wanamuziki waweze kufanikisha malengo yao bila kudhalilishwa kwa misimamo yao ya kisiasa. Cindy, ambaye ni mmoja wa wanamuziki wakongwe na mashuhuri nchini Uganda, amesema nia yake ni kuhakikisha kuwa muziki hauchukuliwi kama kikwazo kwa yeyote anayeamua kujaribu siasa, bali kila taaluma ipewe heshima yake bila kuathiri nyingine.

Read More
 Bien Awaonya Wanaoidharau Maisha ya Ndoa

Bien Awaonya Wanaoidharau Maisha ya Ndoa

Mwanamuziki Bien, kutoka kundi la Sauti Sol, ameweka wazi mtazamo wake kuhusu ndoa akisema kwamba ni jambo zuri na lenye manufaa kwa mtu binafsi na hata kwa jamii. Akipiga stori na SPM Buzz, Bien amesema kuwa licha ya kuwepo kwa mitazamo tofauti kutoka kwa watu wengine, yeye anaamini ndoa inaleta ukuaji wa kweli katika maisha ya mtu. Ameeleza kuwa watu wanaoona ndoa kama mzigo au kizuizi wanakosea, kwani yeye mwenyewe ni mfano hai wa mafanikio na mabadiliko chanya yanayotokana na ndoa yake. Kwa mujibu wa msanii huyo, ndoa siyo kikwazo cha maendeleo kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu, bali ni chanzo cha baraka na chachu ya ukuaji wa mtu binafsi na kifamilia. Kauli ya Bien imekuja baada ya socialite wa Kenya, aitwaye Chebet Rono, kuzua mjadala mitandaoni akidai kuwa ndoa hubamba mafala. Kauli ambayo iliibua hisia mseto, huku watumiaji wa mitandao ya kijamii wakijadiliana kwa mapana kuhusu mustakabali na maana ya ndoa kwa vijana wa kizazi cha sasa.

Read More
 Zuchu Apokea Malipo Yake ya Show ya Fainali za CHAN Kenya

Zuchu Apokea Malipo Yake ya Show ya Fainali za CHAN Kenya

Staa wa muziki kutoka WCB, Zuchu, hatimaye amethibitisha kupokea malipo yake ya onyesho alilolifanya katika fainali za Mashindano ya CHAN yaliyofanyika nchini Kenya. Kupitia ukurasa wake wa Instastory, Zuchu aliandika kuwa anashukuru mashabiki na watu wote waliowezesha ujumbe wake kufika kwa mashirika husika. Alisema kuwa tayari amepokea malipo yake yote na sasa anaendelea mbele na kazi zake. Hii inakuja siku chache baada ya msanii huyo kuibua malalamiko mitandaoni akidai kuwa tangu atumbuize kwenye fainali hizo hakulipwa stahiki zake. Kauli yake ya sasa imeondoa sintofahamu na kuthibitisha kuwa suala hilo limepatiwa suluhisho. Mashabiki wake wamefurahia kuona tatizo hilo limekwisha huku wengine wakimpongeza kwa uthubutu wa kulizungumza waziwazi.

Read More
 Msanii Petra Aolewa Na Mr. Hamza Katika Harusi ya Kuvutia

Msanii Petra Aolewa Na Mr. Hamza Katika Harusi ya Kuvutia

Msanii wa muziki wa rap kutoka Kenya, Petra, ameanza rasmi maisha mapya ya ndoa baada ya kufunga pingu za maisha na mpenzi wake Bw. Hamza katika sherehe ya kifahari iliyofanyika tarehe 14 Septemba 2025 Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Petra alitangaza habari hiyo njema kwa mashabiki wake akipakia picha za harusi na ujumbe wa kugusa moyo uliodhihirisha imani yake kwa Mungu. Alieleza kuwa yeye na mume wake waliombeana mbele za Mungu, na hatimaye wakabarikiwa kuunganishwa kama mume na mke kama ilivyo katika Mathayo 18:19. Katika ujumbe wake, Petra alifafanua pia maana ya jina la Kiebrania Hamza, ambalo tafsiri yake ni “mkono wa ulinzi” unaohusishwa na Jicho la Mungu, ishara ya baraka na kinga ya kiungu. Alisema kwao, jina la Bwana na Bi Hamza ni zaidi ya cheo cha kifamilia, bali ni alama ya agano takatifu lililotiwa muhuri wa ulinzi wa Mungu. Aidha, alimalizia kwa kumshukuru Mungu Mwenyezi, Bwana Yesu Kristo na Roho Mtakatifu kwa kuwa msingi wa ndoa yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni ushuhuda wa neema na utukufu wa Mungu. Tangazo hilo liliibua wimbi la pongezi kutoka kwa mashabiki na wasanii wenzake waliompongeza kwa kuanza ukurasa mpya wa maisha yake kama Bi. Hamza. Harusi hii imekuwa hatua muhimu kwa Petra, ikionyesha sura mpya si tu katika maisha yake ya kifamilia, bali pia katika safari yake ya kiroho na kisanii

Read More
 Maandalizi ya Standard Chartered Marathon Yapamba Moto

Maandalizi ya Standard Chartered Marathon Yapamba Moto

Zaidi ya washiriki 21,000 wamejisajili kufikia sasa kushiriki katika makala ya 22 ya mbio za marathoni za Standard Chartered yatakayoandaliwa tarehe 26 mwezi ujao katika bustani ya Uhuru Gardens jijini Nairrobi. Mwenyekiti wa Kamati andalizi ya mbio hizo David Mwindi ambaye alikuwa akizungumza wakati wa mbio za maandalizi zilizoandaliwa katika Msitu wa Karura anasema wananuia kusajili washiriki wapatao 30,000. Lampard Mutuku alishinda mbio za kilomita 21 wakati wa mbio hizo za maandalizi yaliyowavutia takriban washiriki 1500. Mashindano ya kila mwaka ya marathoni ya Stanchart yanadhamiria kukusanya fedha kwa ajili ya talanta za siku zijazo, mpango wa kimataifa unaowawezesha vijana kupitia elimu, kuajiriwa na ujasiriamali.

Read More
 Diamond Awapa Vijana Somo Zito Kuhusu Mapenzi na Maisha

Diamond Awapa Vijana Somo Zito Kuhusu Mapenzi na Maisha

Staa wa muziki kutoka Tanzania, Diamond Platnumz, ametoa ushauri mzito kwa vijana ambao bado hawajaoa, akiwataka kuacha kudharau miili yao na kupoteza fedha kwa kuwa na wanawake wengi. Kupitia ujumbe aliouandika SnapChat, Diamond amewaonya vijana kwamba tabia ya kubadilisha wapenzi mara kwa mara haiwezi kuwasaidia kufanikisha ndoto zao wala kuwapeleka popote kimaisha. Mwanamuziki huyo amesema kuwa hekima ya kweli ni kujitambua na kuamua kutulia na mpenzi mmoja, au wawili, huku akieleza kuwa kiwango cha juu kabisa kisipite watatu. Aidha, ameongeza kuwa katika hali ya changamoto kubwa, vijana wanaweza kuwa na wanne pekee. Ushauri huo umewavutia mashabiki wengi mitandaoni, huku baadhi wakipongeza msimamo wa Diamond kama njia ya kuhamasisha vijana kuheshimu maisha yao na kutumia rasilimali zao kwa uangalifu.

Read More
 Feffe Bussi: Wasanii Acheni Kutegemea Magenge kwa Ulinzi

Feffe Bussi: Wasanii Acheni Kutegemea Magenge kwa Ulinzi

Msanii wa muziki wa rap kutoka Uganda, Feffe Bussi, ameonyesha kutoridhishwa na mtindo unaokua wa wasanii kuandamana na magenge ya vijana wakorofi, akiwataka wasanii wenzake waajiri walinzi binafsi badala yake. Kwenye mahojiano hivi karibuni, Feffe Bussi ameeleza kuwa magenge hayaleti faida yoyote, bali husababisha vurugu na kuwatishia mashabiki. Amesisitiza kuwa walinzi binafsi wawili wanaweza kutoa ulinzi wa kutosha kwa msanii bila madhara yoyote. Kwa mtazamo wake, utegemezi wa magenge unaharibu taswira ya tasnia ya muziki na hauleti maendeleo yoyote. Anaamini kuwa magenge ni hatari na yanapaswa kuondolewa kabisa kwenye sekta ya burudani ili kuifanya kuwa salama zaidi kwa wasanii na mashabiki. Hivi karibuni, tasnia ya muziki nchini Uganda imeanza kushuhudia wimbi jipya la wasanii kuandamana na makundi makubwa ya watu, hali ambayo imezua mjadala. Miongoni mwao ni Alien Skin, kiongozi wa Fangone Forest, anayejulikana kwa kutembea na zaidi ya watu hamsini. Wengine ni Mudra, Fik Gaza na, hivi karibuni, mwimbaji nguli Jose Chameleone naye amejiunga na mtindo huo.

Read More
 S2kizzy Awahimiza Maprodyuza Kuwa Wajasiri Katika Muziki

S2kizzy Awahimiza Maprodyuza Kuwa Wajasiri Katika Muziki

Prodyuza wa muziki kutoka Tanzania, S2kizzy, amewashauri maprodyuza wenzake kutoogopa kufanya aina yoyote ya muziki kwa kuhofia maneno ya watu. Kwa mujibu wa S2kizzy, muziki ni sanaa ya burudani na furaha, hivyo kila prodyuza ana nafasi ya kujaribu mitindo na miondoko mbalimbali ili kuleta furaha na burudani kwa jamii. S2kizzy, ambaye amehusishwa na kutengeneza hit singles nyingi za wasanii wakubwa Afrika Mashariki, amesisitiza kuwa ubunifu na kujiamini katika kazi ndiyo msingi wa mafanikio katika tasnia ya muziki ambayo imejaa ushindani mkubwa. Ujumbe huu umetafsiriwa kama motisha kwa vijana wengi wanaojitahidi kuingia kwenye muziki lakini hukumbwa na hofu ya mitazamo ya watu

Read More
 Msanii Iyanii Afichua Bado Ni Bikira, Asema Atasubiri Ndoa

Msanii Iyanii Afichua Bado Ni Bikira, Asema Atasubiri Ndoa

Msanii wa muziki kutoka Kenya, Iyanii, amefichua kuwa bado ni bikira na ameamua kuhifadhi ubikra wake hadi atakapoingia kwenye ndoa rasmi na mpenzi wake, Kemunto. Akizungumza katika mahojiano na mtangazaji Alex Mwakideu, Iyanii amesema kuwa yeye na mpenzi wake wamekubaliana kuishi maisha ya kutojihusisha na ngono kabla ya ndoa. Hitmaker huyo “Donjo Maber”, amesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya maadili yake binafsi na pia ni ishara ya heshima kwa mpenzi wake. Iyanii, ameongeza kuwa uamuzi huo pia ni njia ya kuweka msingi imara kwa maisha yake ya kifamilia. Kauli ya msanii huyo imezua mjadala miongoni mwa mashabiki, wengine wakimsifia kwa ujasiri na msimamo wake, huku baadhi wakionesha mshangao kutokana na hadhi yake kama msanii maarufu wa burudani.

Read More
 YouTube Yafungua Mlango Mpya wa Ubunifu Kupitia Akili Bandia

YouTube Yafungua Mlango Mpya wa Ubunifu Kupitia Akili Bandia

Kampuni ya YouTube imetangaza kuanzisha rasmi matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) inayoitwa Veo katika programu na tovuti zake, hatua inayolenga kurahisisha utengenezaji wa video kwa watumiaji wake duniani kote. Kupitia mfumo huu, watumiaji wataweza kutengeneza video kwa kutumia maelezo ya maandishi tu, bila kuhitaji ujuzi wa kina katika uhariri wa video au vifaa maalum vya kitaalamu. Veo ni teknolojia ya hali ya juu inayoweza kutafsiri maelezo mafupi (text prompts) na kuyabadilisha kuwa video za ubora wa juu. Kwa mfano, mtumiaji anaweza kuandika sentensi kama picha ya jua linapotua baharini na AI hiyo kutengeneza video inayolingana na maelezo hayo. YouTube imeeleza kuwa teknolojia hii inalenga kuwasaidia wabunifu wa maudhui wazo likitoka kichwani moja kwa moja hadi kuwa video halisi. Mbali na kutengeneza video mpya, mfumo wa Veo pia utawapa watumiaji uwezo wa kuhariri maudhui yao kwa kutumia sauti au maandishi, pamoja na kupokea mapendekezo ya uhariri kutoka kwa AI hiyo. Hii ni sehemu ya juhudi za YouTube kuendeleza ubunifu na kurahisisha kazi ya wabunifu wa maudhui wa kizazi kipya, bila kuwabana kwa gharama au ujuzi wa kiufundi. Kwa sasa, YouTube imesema mfumo huu utaanza kwa watumiaji wachache walioteuliwa katika kipindi cha majaribio kabla ya kusambazwa kwa watumiaji wote duniani. Wakati wadau wa teknolojia na ubunifu wakipokea habari hii kwa furaha, pia kumekuwepo na mjadala kuhusu nafasi ya binadamu katika uumbaji wa maudhui. Hata hivyo, YouTube imesisitiza kuwa lengo la Veo ni kuongeza ubunifu wa binadamu, si kuubadilisha.

Read More
 Mbio za Moscow Zafungua Fursa Kubwa Kwa Wanariadha

Mbio za Moscow Zafungua Fursa Kubwa Kwa Wanariadha

Makala ya 12 ya mbio za marathoni za Moscow yanatarajiwa kufanyika tarehe 21 mwezi huu katika mji mkuu wa Urusi, huku zaidi ya wanariadha 50,000 wakitarajiwa kushiriki katika mashindano hayo makubwa ya mbio za umbali mrefu. Wanariadha kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, India, China, Kyrgyzstan, Morocco, Belarus, Ethiopia, Afrika Kusini na mengineyo watapambana kwa nguvu zote kuwania ubingwa wa mbio hizo. Mashindano haya yataandaliwa kwa msaada wa Serikali ya Moscow na Idara ya Michezo ya jiji hilo, huku akisisitiza kuendeleza shughuli za michezo katika mkoa huo. Mbio za marathoni za Moscow ni sehemu ya mfululizo wa Ligi ya mbio za marathoni za BRICS, ambapo mwaka huu, wanariadha zaidi ya 1,800 watashiriki kwa mara ya tatu, idadi ambayo ni mara tano zaidi ikilinganishwa na mwaka jana. Zaidi ya washiriki 3,000 watashiriki kwa mara ya pili, jambo ambalo linaonyesha ukuaji mkubwa wa shindano hilo. Tarehe 20 Septemba, siku kabla ya mbio kuu, kutakuwa na mashindano ya mbio za kilomita 10, ambayo pia yamepata umaarufu mkubwa miongoni mwa washiriki kutoka mataifa mbalimbali. Mbio kuu za marathoni zenye umbali wa kilomita 42.2 zitaanza rasmi tarehe 21 Septemba, na zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali kati ya wanariadha walioko katika kiwango bora kimataifa.

Read More