Gossip

Bahati Aingilia Kati Drama ya Mulamwah na Ruth, Atoa Wito wa Amani

Bahati Aingilia Kati Drama ya Mulamwah na Ruth, Atoa Wito wa Amani

Msanii maarufu wa muziki nchini Kenya, Bahati, ametoa wito wa amani na msamaha kwa wasanii wenzake Mulamwah na Ruth K, akiwataka kuweka tofauti zao binafsi mbali na mitandao ya kijamii kwa ajili ya mustakabali wa mtoto wao.

Kupitia ujumbe wa kugusa moyo aliouandika kwenye ukurasa wake wa Instagram, Bahati alisema kuwa hajazoea kuingilia mambo ya watu binafsi, lakini hali inayoshuhudiwa kati ya Mulamwah na Ruth imemsikitisha sana kama mzazi na mwanajamii.

“Siwezi kuingilia sana mambo ya watu binafsi, lakini sipendezwi kuona familia zikivunjika . Naomba umma tuwaombee vijana hawa wawili, na zaidi ya yote, Mungu arejeshe kile walichopoteza wakati wa sakata hili, aponye mioyo yao na amkinge mtoto asiye na hatia,” aliandika Bahati.

Bahati, ambaye pia ni mzazi na mume wa Diana Marua, alisema kuwa ameshindwa kuwapata Mulamwah na Ruth kwa simu, na hivyo kuamua kuwafikia kwa njia ya umma ili kuwataka waepuke kulifanya suala hilo kuwa la hadhara.

“Ombi langu kwa wazazi wenzangu Mulamwah na Ruth (kwa sababu siwezi kuwafikia kwa simu)… tafadhali acheni kuanika haya mitandaoni… ni jambo la kusikitisha lakini naamini litakuwa sawa kwa jina la Yesu .” aliongeza.

Alihitimisha ujumbe wake kwa maandiko ya Biblia kutoka Yakobo 1:20, akisisitiza umuhimu wa kudhibiti hasira wakati wa migogoro ya kifamilia:

“Hasira ya mwanadamu haizai haki ya Mungu,” aliandika Bahati

Kauli ya Bahati imepokelewa kwa hisia kali na wafuasi wake, wengi wakimpongeza kwa kuonesha uelewa na huruma, huku wengine wakitumaini kwamba ujumbe huo utakuwa mwanzo wa mazungumzo ya suluhu kati ya wawili hao.

Hali ya sintofahamu kati ya Mulamwah na Ruth K imekuwa gumzo mitandaoni hapo jana, huku kila mmoja akitoa maelezo yake kuhusu sababu za kutengana kwao, hali ambayo imewaacha mashabiki wakiwa na maoni tofauti.