Gossip

Colonel Mustafa Adai Kuwasaidia Huddah na Noti Flow Kufikia Umaarufu

Colonel Mustafa Adai Kuwasaidia Huddah na Noti Flow Kufikia Umaarufu

Msanii mkongwe wa muziki nchini Kenya,Colonel Mustafa, amezua gumzo mitandaoni baada ya kudai kuwa muda aliowahi kutumia na mastaa wa kike kama Huddah Monroe na Noti Flow uliwasaidia kupenya kwenye anga la umaarufu, wakati walipokuwa bado hawajatambulika sana katika tasnia ya burudani.

Akizungumza kwenye podcast ya Alex Mwakideu Live, alisema kwamba mahusiano yake na wanawake hao yalimsaidia kuwapa mwanga wa mafanikio waliokuwa bado hawajaufikia kwa wakati huo. Kwa mujibu wa msanii huyo, jina lake lilihusishwa na mastaa hao kabla ya wao kung’aa, na hivyo mchango wake haupaswi kupuuzwa.

Kauli hiyo imeibua hisia mseto mitandaoni. Wapo wanaoamini kuwa Mustafa alikuwa sehemu ya safari ya mafanikio ya Huddah na Noti Flow, huku wengine wakimtuhumu kwa kujitafutia kiki na kutumia majina ya watu maarufu kurudi kwenye ramani ya burudani.

Hadi sasa, Huddah Monroe na Noti Flow hawajajibu madai hayo, lakini mashabiki wanazidi kufuatilia kwa makini endapo wahusika watajitokeza kuweka wazi upande wao wa simulizi hii.

Mustafa, anayekumbukwa kwa kazi zake akiwa na kundi la Deux Vultures, anaonekana kurejea tena kwenye vyombo vya habari si kwa muziki, bali kwa matamshi yenye utata kuhusu mahusiano ya zamani.