Staa wa muziki kutoka nchini Uganda, Eddy Kenzo, amewajibu vikali wakosoaji wake baada ya kujipata katika malumbano ya kisiasa na kijamii kufuatia ushiriki wake katika uzinduzi wa albamu ya Rais Yoweri Museveni na kampeni za chama tawala cha NRM.
Kwenye mahojiano yake na kituo kimoja cha redio nchini humo, Kenzo amesema hatatishwa na propaganda wala chuki kutoka kwa wale wanaopinga mafanikio yake, akisisitiza kuwa ataendelea kufanya kazi kwa bidii kuendeleza sekta ya muziki wa Uganda.
Msanii huyo, ambaye ni mwenyekiti wa Uganda National Musicians Federation (UNMF), amesema ataendelea kusimamia umoja na maendeleo ya wasanii wote bila kubagua, akisisitiza kuwa mafanikio yake hayatatetereka kwa sababu ya chuki au upotoshaji.
Hata hivyo, hatua yake ya kushirikiana kwa karibu na serikali imezua chuki kutoka kwa baadhi ya wasanii na mashabiki wanaomuona kama msanii anayependelea chama tawala na kuwapuuza wasanii wakubwa katika tasnia ya muziki. Wengine wameenda mbali zaidi na kumtuhumu kwa kuwapendelea wasanii fulani chini ya UNMF, jambo linalochochea zaidi ukosoaji na propaganda dhidi yake.