Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kuonyesha maendeleo ya ujenzi wa nyumba yake ya kifahari ya ghorofa.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, bosi huyo wa lebo ya Konde Gang amepost video fupi (clip) akionekana akikagua mjengo wake mpya unaoendelea kujengwa. Katika clip hiyo, Harmonize anaonekana akitembea ndani na nje ya jengo hilo huku akitazama hatua mbalimbali za ujenzi.
Licha ya kutoweka maelezo yoyote kwenye posti hiyo, Harmonize ametumia wimbo wake “I Made It” kama muziki wa background, jambo ambalo mashabiki wengi wametafsiri kuwa ni ishara ya kujivunia mafanikio yake binafsi pamoja na hatua ya mwisho ya kukamilika kwa mjengo huo.
Hatua hiyo imewakumbusha wengi kauli ya Harmonize aliyotoa miaka kadhaa iliyopita alipodokeza kuwa alikuwa mbioni kujenga nyumba ya ghorofa. Wakati huo, baadhi ya watu walichukulia kauli hiyo kama mzaha, lakini sasa msanii huyo ameonekana kuthibitisha kuwa ndoto yake ilikuwa ya kweli.