Msanii wa muziki na mjasiriamali kutoka Tanzania, Shilole, amefunguka kuhusu tukio la kusikitisha la kuchomwa kwa mgahawa wake, Shishi Food, wakati wa machafuko yaliyojitokeza katika kipindi cha uchaguzi nchini Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Shilole amesema licha ya hasara kubwa aliyopata, hana chuki wala kinyongo dhidi ya waandamanaji waliohusika na uharibifu huo. Kwa mujibu wake, waandamanaji hao ni wananchi waliokuwa wamechoka na hali mbalimbali, hivyo haoni sababu ya kuwachukia.
Msanii huyo ameeleza kuwa tukio hilo limezidisha ari yake ya kupambana na kusimama imara zaidi. Amesema yeye ni kijana mpambanaji na changamoto hiyo imempa nguvu mpya ya kuendelea kujijenga upya na kusonga mbele katika maisha na biashara.
Shilole ameongeza kuwa licha ya maumivu ya kupoteza alichokijenga kwa jasho, hawezi kukata tamaa, akisisitiza kuwa bado ana ndoto kubwa na dhamira ya kufanikiwa zaidi.