Msanii mkongwe wa muziki nchini Kenya, Prezzo, ametoa wito kwa mapromota wa burudani nchini humo kuzingatia ombi la msanii DNA, akiwataka kumpatia nafasi ya kushiriki kwenye shows za kufunga mwaka, hususan zile za tarehe 31 Desemba.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Prezzo amewaomba mapromota kuonyesha moyo wa kusaidia, akisema kuwa DNA haombi mengi, bali dili ya maana itakayomuwezesha kufunga mwaka kwa heshima.
Wito huo unakuja baada ya DNA kujitokeza hadharani na kueleza kilio chake, akiomba kuzingatiwa katika maonesho hayo muhimu ya mwisho wa mwaka. Msanii huyo alidai kuwa kwa muda sasa amekuwa akifungiwa milango kwenye tasnia ya burudani kutokana na kutoelewana na baadhi ya wadau, hali iliyomwathiri kiuchumi na kikazi.
Hatua ya Prezzo imeonekana kama ishara ya mshikamano ndani ya tasnia ya muziki, ikilenga kuhakikisha vipaji havizimwi kutokana na migogoro ya muda mrefu. Wengi sasa wanasubiri kuona iwapo mapromota wataitikia wito huo na kumpatia DNA nafasi ya kuonesha kipaji chake kwenye jukwaa kubwa la kufunga mwaka.