Entertainment

Ibraah Atangaza Kuondoka Rasmi Konde Gang Baada ya Kikao na BASATA

Ibraah Atangaza Kuondoka Rasmi Konde Gang Baada ya Kikao na BASATA

Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Ibrahim Abdallah maarufu kama Ibraah, ametangaza rasmi kuondoka kwenye lebo ya Konde Music Worldwide baada ya kikao cha mwisho kilichowahusisha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pamoja na uongozi wa lebo hiyo.

Kupitia mahojiano baada ya kikao hicho, Ibraah amethibitisha kuwa wamefikia mwafaka wa kumaliza tofauti zao na uongozi wa Konde Gang. Hata hivyo, ameeleza kuwa bado hajakabidhiwa baadhi ya vitu muhimu vinavyohusiana na kazi yake ya muziki, ikiwemo akaunti zake za digital platforms kama YouTube, Boomplay, na Spotify.

Kwa upande wao, uongozi wa Konde Gang kupitia Sandra, ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa lebo hiyo, wamethibitisha kuwa Ibraah atakabidhiwa rasmi akaunti hizo kabla ya mwisho wa leo. Aidha, Sandra amemtakia kila la heri Ibraah katika safari yake mpya ya muziki nje ya Konde Gang, akisisitiza kuwa hakuna uadui kati yao bali ni mabadiliko ya kawaida katika tasnia ya sanaa.

Kuondoka kwa Ibraah kunakuja baada ya muda mrefu wa tetesi na hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wake ndani ya Konde Gang. Mashabiki wake sasa wanangoja kwa hamu kuona ni wapi atapeleka kipaji chake na iwapo ataendelea kung’ara kama msanii huru.

Hii ni miongoni mwa migogoro ya kimikataba inayozidi kuibuka katika tasnia ya muziki Tanzania, huku mashirika kama BASATA yakihimiza mazungumzo ya kidiplomasia kama njia ya kutatua mizozo kati ya wasanii na lebo zao. Ibraah alikuwa msanii wa kwanza kusainiwa Konde Music mwaka 2020, na ametoa nyimbo kadhaa zilizotikisa chati za muziki Afrika Mashariki, kama vile One Night Stand, Nani, na Dharau akiwa chini ya lebo hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *