
Mwanamuziki maarufu na mwanasiasa chipukizi, Nina Roz, ameibua mjadala mpya katika tasnia ya muziki nchini Uganda baada ya kufichua sababu zilizomfanya kujiondoa kwenye Shirikisho la Kitaifa la Wanamuziki nchini humo (UNMF)
Katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni na vyombo vya habari, Nina Roz alieleza kuwa walibuni shirikisho hilo pamoja na Eddy Kenzo kwa madhumuni ya kuwatetea wasanii, kusimamia haki zao, na kuendeleza ustawi wa sekta ya muziki nchini Uganda. Hata hivyo, alidai kuwa hali hiyo ilianza kubadilika muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa shirikisho hilo mwaka 2023.
“Nilidhani tunaunda jukwaa la kweli la kuwaunganisha wasanii na kuwatetea, lakini baadaye nikabaini kuwa viongozi, hususan Eddy Kenzo, walikuwa na maslahi binafsi pamoja na ajenda za kisiasa ambazo hazikuwiana na malengo ya awali,” alisema Nina Roz.
Nina, ambaye aliwahi kushika wadhifa wa kusimamia masuala ya maadili ndani ya UNMF, alieleza kuwa shirikisho hilo lilianza kupoteza dira na kuonyesha ukaribu usiofaa na serikali. Kwa maoni yake, hali hiyo ilikuwa kinyume na misingi ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa kisanii.
Tangu kujiondoa kwake, Nina Roz amekuwa mkosoaji wa wazi wa shirikisho hilo, akilituhumu kwa kile alichokitaja kuwa ni siasa za upendeleo katika tasnia ya muziki. Anadai kuwa wasanii wanaoonekana kukosoa serikali wamekuwa wakibaguliwa katika upatikanaji wa fursa, mikataba, na msaada kutoka kwa taasisi hiyo.
“UNMF haikuwakilisha tena maslahi ya wasanii wote. Iligeuka kuwa jukwaa la upande mmoja, ambapo wale waliokuwa karibu na serikali ndio walipewa kipaumbele,” aliongeza.
Kwa sasa, Nina Roz anajiunga na orodha ya wasanii wakubwa kama King Saha, Ziza Bafana, na Spice Diana, ambao wote wamejitenga na UNMF, wakieleza kutoridhishwa na namna taasisi hiyo inaendeshwa.