Bebe Cool Aeleza Sababu ya Wasanii wa Afrika Mashariki Kusalia Nyuma Kisanaa

Bebe Cool Aeleza Sababu ya Wasanii wa Afrika Mashariki Kusalia Nyuma Kisanaa

Mwanamuziki mkongwe kutoka Uganda, Bebe Cool, ameonyesha masikitiko yake kuhusu hali ya muziki wa Afrika Mashariki, akieleza kuwa miaka 15 iliyopita wasanii wa ukanda huo walikuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kimataifa lakini walikosa kuendeleza juhudi hizo. Kwa mujibu wa Bebe Cool, kipindi hicho kulikuwa na umaarufu mkubwa ambao ulipaswa kutumiwa kama daraja la kuingia katika soko la kimataifa. Hata hivyo, anasema wasanii wengi waliridhika mapema na kupoteza ari ya kusonga mbele. Ametoa mfano wa wasanii kutoka Nigeria ambao waliendelea kusukuma juhudi zao na sasa wamefanikiwa kutamba duniani, huku wenzao wa Afrika Mashariki wakibaki nyuma. “Miaka 15 iliyopita tulikuwa juu sana, lakini hatukuitumia nafasi hiyo vizuri. Wasanii wa Afrika Mashariki tuliridhika, tukakata tamaa, huku wenzao wa Nigeria wakiendelea kusonga mbele,”  Alisema akizungumza na runinga ya K24. Kauli yake imeibua mijadala mitandaoni, wengi wakimtaka kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kushirikiana na wasanii wachanga ili kufufua na kuimarisha muziki wa Afrika Mashariki. Lakini pia wametoa wito kwa wasanii wa ukanda huo kurejea katika ushindani wa kimataifa kwa kujifunza kutoka kwa mafanikio ya wasanii wa Nigeria kama Burna Boy, Wizkid, na Davido. Bebe Cool anahesabiwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya katika ukanda huu, akiwa na mchango mkubwa katika kukuza dancehall na reggae.

Read More
 Bebe Cool Afichua Lengo la Ziara Yake ya Siku 7 Nchini Kenya

Bebe Cool Afichua Lengo la Ziara Yake ya Siku 7 Nchini Kenya

Mwanamuziki nguli kutoka Uganda, Bebe Cool, amefichua kuwa ziara yake ya siku saba nchini Kenya inalenga zaidi kushirikiana na wasanii wa humu nchini na kujenga mahusiano mapya katika tasnia ya muziki wa Afrika Mashariki. Akizungumza wakati wa mahojiano  jijini Nairobi, Bebe Cool alieleza kuwa anatamani kufanya kazi na wasanii wakubwa wa Kenya akiwemo Bien wa Sauti Sol, pamoja na wanamuziki waliotamba kwa miaka mingi kama Wyre na Nazizi. “Kenya ni nyumbani kwangu. Muziki wetu wa Afrika Mashariki unaweza kuimarika zaidi tukishirikiana. Niko hapa kwa wiki moja lakini nina malengo ya muda mrefu, si tu collabo moja,” alisema Bebe Cool kwa msisitizo. Mbali na wasanii, Bebe Cool pia alionyesha nia ya kufahamiana na DJs wapya wa Kenya, akisema wao ni kiungo muhimu katika kusukuma muziki wa kanda hii kimataifa. Mashabiki wa muziki wa Afrika Mashariki wamepokea taarifa hiyo kwa furaha, wengi wakitarajia mashirikiano ya kuvutia ambayo yatabeba ladha ya muziki wa Kenya na Uganda. Wadau wa burudani wanasema hatua hiyo inaweza kufungua milango ya ushawishi wa kimataifa kwa wasanii wa eneo hili.

Read More
 Bebe Cool Asema Mwanawe Allan Hendrick Anakumbwa na Changamoto za Afya ya Akili

Bebe Cool Asema Mwanawe Allan Hendrick Anakumbwa na Changamoto za Afya ya Akili

Msanii maarufu wa muziki wa Uganda, Bebe Cool, amefunguka na kuthibitisha kuwa mwanawe Allan Hendrick anapambana na changamoto za afya ya akili. Ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusu hali hiyo, amesisitiza kuwa ni jukumu la mwanawe mwenyewe kushinda na kuweza kushughulikia matatizo hayo binafsi. Katika mahojiano na vyombo vya habari, Bebe Cool alieleza kuwa changamoto hizo ni za kibinafsi na zilimfikia Allan kwa kiwango ambacho hata familia na marafiki walishindwa kumpa msaada wa kutosha. “Ni kweli Allan alikuwa anakumbwa na changamoto binafsi ambazo mimi au mtu mwingine hatukuweza kumsaidia kutoka kwao.” Alisema Bebe Cool. Taarifa hii imeibua hisia mchanganyiko kutoka kwa mashabiki na wafuasi wake, wengi wakimwombea nguvu na kuonyesha mshikamano kwa Allan. Afya ya akili ni changamoto inayogusa watu wengi duniani, na kuzungumzia hadhi hii wazi ni hatua muhimu katika kupambana na unyanyapaa unaozunguka. Watu maarufu kama Bebe Cool wanachukuliwa kuwa nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko chanya kwa kuzungumza hadharani kuhusu masuala haya nyeti.

Read More
 Gravity Omutujju Atangaza Mapenzi Hadharani Kwa Mke wa Bebe Cool

Gravity Omutujju Atangaza Mapenzi Hadharani Kwa Mke wa Bebe Cool

Msanii maarufu wa muziki wa Hip Hop nchini Uganda, Gravity Omutujju, amezua gumzo mitandaoni baada ya kukiri wazi kuwa ana hisia za kimapenzi kwa Zuena Kirema, mke wa mwanamuziki mashuhuri Bebe Cool. Katika mahojiano na TikToker mmoja maarufu, Gravity alifunguka kwa mara ya kwanza kuhusu hisia zake kwa Zuena, akieleza kuwa amekuwa na “crush” naye kwa muda mrefu, na licha ya ndoa ya Zuena na Bebe Cool kuwa imara, bado anampenda kisiri. “Sijawahi kumuambia lakini ukweli ni kwamba nina ‘crush’ naye. Ni mwanamke mrembo sana, na hata kama ameolewa, siwezi kuficha hisia zangu,” alisema Gravity kwa ucheshi. Zuena Kirema, ambaye ameolewa na Bebe Cool kwa zaidi ya muongo mmoja na wana watoto pamoja, hajatoa tamko lolote kuhusu kauli hiyo ya Gravity. Bebe Cool pia hajaonekana kuguswa moja kwa moja na taarifa hiyo, ingawa mashabiki wake wengi wameonyesha mshtuko na wengine kuchukulia kama mzaha wa kawaida wa mastaa.

Read More
 Bebe Cool Azua Gumzo Baada ya Kuwekeza $700K Kwenye Album Mpya

Bebe Cool Azua Gumzo Baada ya Kuwekeza $700K Kwenye Album Mpya

Msanii maarufu wa muziki nchini Uganda, Bebe Cool, amefunguka kuhusu maswali yanayoendelea kuibuka kuhusu uwekezaji mkubwa alioufanya katika utengenezaji wa album yake mpya yenye nyimbo 16. Msanii huyo amefichua kuwa amewekeza zaidi ya dola 700,000 za Kimarekani kwenye mradi huo.Akizungumza na waandishi wa habari, Bebe Cool, ambaye jina lake halisi ni Moses Ssali, amesisitiza kuwa kiasi hicho cha fedha kimetumika ipasavyo kuhakikisha ubora wa hali ya juu wa album hiyo.Msanii huyo hakusita kuwajibu wale wanaotia shaka kiasi hicho cha fedha, akieleza kuwa gharama hizo zinajumuisha mambo mengi kuanzia kurekodi nyimbo katika studio za kisasa, malipo kwa watayarishaji wa muziki (producers) maarufu, uhandisi wa sauti (audio engineering), video za muziki zenye ubora wa hali ya juu, pamoja na gharama za masoko na matangazo.Album hiyo ya nyimbo 16 inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni, na tayari imezua hamasa kubwa miongoni mwa mashabiki wake na wadau wa muziki. Bebe Cool ana matumaini kuwa uwekezaji huu utalipa na kumpa nafasi nzuri zaidi kwenye tasnia ya muziki ya kimataifa..

Read More
 Bebe Cool Aomba Msaada wa Rais Kutangaza Albamu yake Mpya Kimataifa

Bebe Cool Aomba Msaada wa Rais Kutangaza Albamu yake Mpya Kimataifa

Msanii maarufu wa Uganda na mwanzilishi wa Gagamel Crew, Bebe Cool, ametangaza kuwa albamu yake mpya “Break the Chains” itazinduliwa rasmi tarehe 30 mwezi huu. Albamu hiyo, ambayo ni ya saba katika kazi yake ya muziki, imechukua karibu mwaka mmoja kuikamilisha na imerekodiwa katika studio za kimataifa nchini Nigeria, Afrika Kusini, na Uingereza. Katika mahojiano na televisheni ya ndani, Bebe Cool alifichua kuwa hadi sasa ametumia zaidi ya shilingi bilioni 2.56 za Uganda katika utayarishaji wa albamu hiyo, ikijumuisha gharama za uandishi wa nyimbo, uzalishaji, mastering, na posho kwa timu yake ya uzalishaji ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto kubwa sasa ni kuisambaza na kuitangaza kimataifa, jambo ambalo litahitaji zaidi ya shilingi bilioni 7 (takriban dola milioni 2). “Mpaka sasa nimetumia dola 700,000. Kufanya muziki wa kiwango cha juu kunahitaji uwekezaji mkubwa. Ili niweze kuitangaza albamu hii kimataifa, nitahitaji zaidi ya dola milioni 2. Nampasa Rais Museveni kuniunga mkono katika hili,” alieleza Bebe Cool. Kwa msingi huo, Bebe Cool ameeleza kuwa anatafuta msaada wa kifedha kutoka kwa Rais Yoweri Kaguta Museveni, ili kufanikisha azma ya kuitangaza albamu hiyo katika soko la kimataifa. Anaamini “Break the Chains” itaweka muziki wa Uganda kwenye ramani ya dunia, na kuwa kichocheo kwa wasanii wengine kuwekeza katika kazi zao kwa maendeleo ya sekta nzima ya burudani nchini.

Read More
 Eddy Kenzo Apuzilia Mbali Madai ya Bebe Cool ya Kudhibiti Muziki

Eddy Kenzo Apuzilia Mbali Madai ya Bebe Cool ya Kudhibiti Muziki

Msanii nyota wa Uganda, Eddy Kenzo, ameibuka na kauli kali dhidi ya madai ya Bebe Cool kwamba yeye hudhibiti namna nyimbo zinavyopigwa kwenye redio na runinga nchini humo. Kenzo, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kimataifa kutoka Afrika Mashariki, amesema Bebe Cool hana ushawishi mkubwa kama anavyodai. “Bebe Cool hana uwezo wa kudhibiti airplay kama anavyodhani. Sisi tulipata mafanikio makubwa wakati yeye bado yupo kwenye tasnia, kwa hiyo kauli zake hazina uzito wowote,” alisema Kenzo katika mahojiano na msanii Vampino. Kauli hii ni majibu ya moja kwa moja kwa matamshi ya Bebe Cool aliyotoa mwezi Aprili, ambapo alijisifu kuwa ana ushawishi mkubwa kwenye vituo vya habari na anaweza kuzuia wimbo wowote usipigwe Uganda. “Mimi si rafiki tu wa DJs, bali pia wa wamiliki wa vituo vya redio na TV. Naweza kuamua wimbo gani usipigwe popote nchini,” alisema Bebe Cool awali, akidai wasanii wachanga wanafaa kumheshimu kama mlezi wa tasnia. Lakini kwa Eddy Kenzo, mafanikio hayatokani na upendeleo au vitisho vya watu maarufu bali kutokana na bidii, kipaji na kujituma kwa msanii binafsi. “Wasanii wapya wasihangaike na matamshi kama haya. Wajikite kwenye kazi yao. Mafanikio hayaletiwi na maneno ya mtu bali kazi nzuri,” alisisitiza Kenzo. Bifu hili la kauli kati ya mastaa hawa wawili linaashiria mvutano mkubwa wa ushawishi ndani ya tasnia ya muziki nchini Uganda, huku mashabiki wakigawanyika kati ya kuunga mkono upande wa Kenzo au Bebe Cool. Lakini kwa sasa, Kenzo ameweka wazi msimamo wake kwamba hana muda wa kuendekeza maneno yasiyo na msingi.

Read More
 King Saha akanusha madai ya kutumia mihadarati.

King Saha akanusha madai ya kutumia mihadarati.

Mwanamuziki kutoka nchini Uganda King Saha amejitenga na madai yaliyoibuliwa na Bebe Cool kuwa anatumia mihadarati. Kwenye mahojiano yake hivi karibuni amesema alihasi matumizi ya dawa za kulevya miaka mingi iliyopita baada ya kugundua kuwa inaathari afya yake. Hitmaker huyo wa “Zakayo”, ameanika tusiyojua kuhusu Bebe Cool kwa kusema kuwa msanii huyo anatumia bangi pamoja na miraa huku akiongeza kuwa alimfunza jinsi ya kutumia dawa za kulevya kipindi cha nyuma. Hata hivyo ametishia kumshambulia Bebe Cool iwapo hataacha tabia ya kumchafulia jina kwenye vyombo vya habari kwa kusema kuwa ana nyimbo nyingi ambazo zipo studio kwa ajili kuanika maovu yote ambayo bosi huyo wa Gagamel amekuwa akifanya kwa siri. King Saha ambaye juzi kati aliondoka hospitalini ambako alikuwa amelazwa baada ya kuugua ugonjwa usiojulikana, atasalia nyumbani kwa wiki mbili zijazo kwa ajili kujiweka sawa kiafya.

Read More
 Eddy Kenzo ajibu madai ya Bebe Cool kuwa amebebwa na bahati kwenye muziki

Eddy Kenzo ajibu madai ya Bebe Cool kuwa amebebwa na bahati kwenye muziki

Nyota wa muziki nchini Uganda Eddy Kenzo amejibu madai ya Bebe Cool kuwa bahati ndio imembeba kwenye muziki. Kwenye mahojiano yake hivi karibuni Kenzo amesema Bebe Cool anatumia madai hayo kujifariji huku akidai kuwa bidii ndio imempa mafanikio makubwa kwenye muziki wake kwa miaka 10 na sio bahati kama namna ambavyo Bosi huyo wa Gagamel anavyodai. Hitmaker huyo wa “Nsimbudde” amesema Bebe Cool anapaswa kukubali kuwa ameacha alama kwenye tasnia ya muziki nchini Uganda badala ya kuwahada mashabiki na taarifa za uongo. “Bebe Cool alisema nina bahati kwa sababu alitaka kujifariji. Huwezi kuwa na bahati milele, najua ninachofanya na nimestahili kile nilichonacho. Anapaswa kukubali na kuwaambia watu wake kwamba Kenzo amefanya muziki kwa zaidi ya miaka 10 na anafahamu hilo,” alisema Eddy Kenzo. Kauli ya Eddy Kenzo inakuja mara baada ya Bebe Cool kuachia orodha ya wasanii waliofanya vizuri mwaka 2022 ambapo alimtaja Kenzo kama msanii aliyebebwa na bahati kwenye muziki.

Read More
 Bebe Cool Alinisaidia Kupata Mawakili katika kesi dhidi ya Luba Events – Eddy Kenzo

Bebe Cool Alinisaidia Kupata Mawakili katika kesi dhidi ya Luba Events – Eddy Kenzo

Msanii Eddy Kenzo amekiri kwamba Bebe Cool alimsaidia kuondokana na kesi iliyokuwa ikimuandama kutoka kwa Luba Events. Katika mahojiano yake hivi karibuni, Kenzo amesema Bebe Cool alimuunganisha na mawakili walioshughulikia kesi yake dhidi ya promota huyo. “Alinipigia simu na kuniuliza anawezaje kusaidia. Hakutaka kuniona nikiwa kwenye matatizo. Ni rafiki wa kweli,” alisema. Utakumbuka Luba Events alimburuza mwimbaji huyo wa ‘Tweyagale’ mahakamani Novemba mwaka 2022 baada ya tamasha la ‘Eddy Kenzo’ kufanya vizuri, akimtuhumu kuvunja mkataba wa kuandaa Tamasha hilo. Luba alieleza kuwa alipata hasara ya takriban shillingi millioni 9 ambayo aliwekeza katika tamasha hilo mwaka 2020. Kenzo alipigwa marufuku kwa muda kutumbuiza jijini Kampala kabla ya marufuku hiyo kuondolewa na mahakama. Utakumbuka Eddy Kenzo na Bebe Cool walianza kuwa marafiki baada ya Kenzo kuwa karibu na chama cha NRM, mrengo wa kisiasa ambao Bebe Cool anaunga mkono.

Read More
 Eddy Kenzo sio gwiji wa muziki – Bebe Cool

Eddy Kenzo sio gwiji wa muziki – Bebe Cool

Msanii Bebe Cool amedai kwamba Eddy Kenzo hana vigezo vya kuitwa lejendari kwenye tasnia ya muziki nchini Uganda. Kwenye mahojiano hivi karibuni amesema hitmaker huyo wa “Nsimbudde” ana mengi ya kufanya kwenye muziki kama kweli anataka kufikia hadhi ya kuitwa nguli. Bosi huyo wa Gagamel anasema Eddy Kenzo ni msanii mwenye bahati tu na anaweza kushinda tuzo ya Grammy mwaka 2023. “Eddy Kenzo ni mwanamuziki mzuri lakini hajavuka mstari wa kuitwa nguli, hata kwa tuzo alizoshinda. Inabidi atie bidii zaidi ili kufikia viwango vya Chameleone, Bobi Wine, na mimi mwenyewe. Sio tu kwa nyimbo na tuzo,” alisema. Utakumbuka juzi kati, Bebe Cool alitoa orodha yake ya kila mwaka ya wasanii waliofanya vizuri mwaka 2022. Bebe Cool aliwataja wanamuziki anaoamini wamepata hadhi ya kuitwa malejendari kwenye kiwanda cha muziki nchini Uganda. Kwenye orodha hiyo aliwataja; Jose Chameleone, Bobi Wine, Afrigo Band, na Maddox Sematimba huku akisisitiza kuwa wanaweza kukaa bila kutoa wimbo mkali kwa miaka mingi ijayo kutokana nyimbo zisizochuja walizoziachia miaka ya hapo nyuma.

Read More
 Nilitabiri Spice Diana atapata mafanikio makubwa kwenye muziki – Bebe Cool

Nilitabiri Spice Diana atapata mafanikio makubwa kwenye muziki – Bebe Cool

Bosi wa label ya Gagamel, Msanii Bebe Cool anasema alikuwa amemtabiria mema Spice Diana kipindi anatoka kimuziki miaka minane iliyopita. Bebe Cool amesema alikuwa anajua mrembo huyo atakuwa mwanamuziki mwenye mafanikio zaidi nchini Uganda bila usaidizi wowote wa staa mkubwa nchini humo. Aidha amefafanua sababu za kukataa kufanya kolabo na Spice Diana kwa kusema kuwa ilikuwa njia ya kumpa changamoto aendelee kuipambania brand yake hadi atakapoachia wimbo mkali kama msanii wa kujitegemea. “Miaka minane iliyopita, Spice Diana na meneja wake walikuja kwangu wakiomba kolabo. Tulikutana kwenye baa moja mjini Ntinda. Nilimwambia afanye kazi kwa bidii hadi atakapoachia wimbo mkali bila usaidizi wa mtu yeyote,” Bebe Cool alielezea. Hata hivyo anaamini ikitokea wamefanya kazi ya pamoja na Spice Diana watafaidi wote kwa kuwa mrembo huyo ameacha alama kwenye kiwanda cha muziki nchini Uganda kutokana na nyimbo ambazo amekuwa akiaziachia katika miaka ya karibuni.

Read More