Duka la Willy Paul Lavamiwa na Watu Wasiojulikana
Staa wa muziki kutoka Kenya, Willy Paul, amethibitisha kuwa duka lake la pombe lilivamiwa usiku wa kuamkia leo na kundi la watu waliodaiwa kukodiwa, ambao waliiba vinywaji vya bei ghali na kuharibu mali nyingi. Kupitia taarifa aliyoitoa kwenye mitandao ya kijamii, Willy Paul amesema wavamizi hao walijaribu kuonesha kana kwamba tukio hilo lilitekelezwa na wanafunzi, ilhali lengo lao kuu lilikuwa ni wizi. Amesema wavamizi hao walivunja madirisha, wakaingia dukani, wakaiba pombe za bei ghali na hata kujaribu kuondoa CCTV hard drive ili kuficha ushahidi, lakini walishindwa. Msanii huyo alieleza kuwa wahalifu hao waliharibu mali nyingi ikiwemo gari lake, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Amesema wanashirikiana kwa karibu napolisi ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Licha ya tukio hilo, hitmaker huyo wa “Ngunga” amewahakikishia mashabiki wake na wateja kwamba biashara yake inaendelea kama kawaida na amewashukuru wote kwa kuendelea kumuunga mkono katika kipindi hiki kigumu.
Read More