
Mastaa wawili wa muziki wa hip hop, Young Thug na Kid Cudi, wameingia kwenye mzozo wa wazi baada ya Cudi kuonekana mahakamani kutoa ushahidi unaomkabili rapa nguli Sean “Diddy” Combs, katika kesi inayohusisha tuhuma za unyanyasaji, ukatili na matumizi mabaya ya madaraka.
Kupitia chapisho aliloliweka kwenye akaunti yake ya X (zamani Twitter), Young Thug aliandika neno “rat” huku akimtag Kid Cudi, kauli ambayo katika muktadha wa mitaani na muziki wa hip hop humaanisha msaliti au mtu anayewasaliti wenzake kwa kushirikiana na vyombo vya sheria. Ingawa Thug alifuta chapisho hilo muda mfupi baadaye, tayari liliwasha moto mitandaoni, huku mashabiki wakitofautiana kuhusu uhalali wa hatua hiyo.
Kid Cudi alionekana kizimbani mwishoni wiki jana kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Diddy, msanii na mfanyabiashara mwenye ushawishi mkubwa katika tasnia ya muziki wa Marekani. Taarifa zinasema ushahidi wa Cudi unahusiana na matukio ya zamani ambayo huenda yakawa na uzito mkubwa katika uamuzi wa mwisho wa kesi hiyo.
Young Thug, ambaye kwa sasa naye anakabiliwa na kesi kubwa ya RICO (Racketeer Influenced and Corrupt Organizations Act) inayohusisha mashitaka ya uhalifu wa genge, ameonekana kuchukulia hatua ya Cudi kama ukiukaji wa kanuni za mtaa, zinazokataza kushirikiana na mamlaka au kutoa ushahidi dhidi ya wenzako.
Wachambuzi wa masuala ya burudani wanasema huenda Thug anaangalia hali hiyo kwa jicho la mtu anayepitia mchakato wa kisheria na kuona kwamba hatua kama ya Cudi zinaweza kudhuru watu walioko kwenye mazingira kama yake.
Kauli ya Thug imezua mijadala mikubwa, huku upande mmoja wa mashabiki ukimtetea Kid Cudi kwa kusema kwamba hatua yake ni ya kijasiri na inalenga kusaidia kutendeka kwa haki. Wengine wanasema Cudi amevunja misingi ya mshikamano katika jamii ya hip hop kwa “kuwageuka” wenzake.
Mpaka sasa, Kid Cudi hajajibu moja kwa moja tuhuma au kejeli hizo kutoka kwa Young Thug. Vyanzo vya karibu na msanii huyo vinaeleza kuwa ameweka mkazo kwenye ukweli na kutafuta haki kwa waathirika.