Msanii nyota wa Uganda, Spice Diana, ameweka wazi kuwa yupo kwenye uhusiano wa kimapenzi lakini ameamua kuficha kwa sasa hadi pale atakapokuwa tayari kuuthibitisha rasmi mbele ya umma.
Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini Uganda, Spice Diana amesema kuwa anafurahia maisha yake ya mapenzi kwa utulivu mkubwa, mbali na macho ya umma. Amebainisha kuwa ni marafiki wachache wa karibu pekee wanaofahamu undani wa uhusiano huo.
Msanii huyo ameeleza kuwa ataamua kumtambulisha mpenzi wake hadharani pale tu atakapokuwa tayari kuchukua hatua kubwa zaidi maishani, ikiwemo kuthibitisha rasmi mipango ya ndoa. Amesema hapendi shinikizo la umma linapokuja suala la mapenzi, jambo linalomfanya awe makini zaidi kabla ya kutoa taarifa kwa mashabiki.
Kauli hiyo ya Spice Diana inakuja wiki kadhaa baada ya tetesi kuzagaa mitandaoni zikidai kuwa msanii huyo alivishwa pete ya uchumba kwa siri akiwa nchini Uingereza. Hata hivyo, msanii huyo hakuthibitisha wala kukanusha moja kwa moja taarifa hizo, akisisitiza kuwa mambo ya mapenzi yanahitaji muda na faragha.