Mchekeshaji na mwanaharakati kutoka nchini Kenya, Eric Omondi, ameendelea kuthibitisha nafasi yake kama sauti ya wananchi baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo ya People’s Champion of the Year katika hafla ya NGO Awards 2025.
Tuzo hiyo, ambayo hutolewa kwa mtu anayejitolea kupigania haki, ustawi na maslahi ya jamii, imeonekana kuwa uthibitisho wa juhudi za Eric katika kuhamasisha wananchi, kufanya harakati za kijamii, na kusaidia watu wenye uhitaji kupitia kampeni zake mbalimbali.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Eric Omondi amewashukuru mashabiki wake akisisitiza kuwa ushindi huo ni wao. Katika ujumbe wake, ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na sapoti na umoja wa mashabiki na wafuasi wake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakimuunga mkono.
Ushindi huu unakuja wakati ambapo Eric Omondi ameendelea kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kijamii, ikiwemo kusaidia familia zisizojiweza, kupigania huduma bora, na kuibua mijadala kuhusu changamoto zinazowakumba wananchi wa kawaida.