Mwimbaji maarufu wa muziki wa R&B, Akon, anakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisheria na kifedha baada ya mke wake, Tomeka Thiam, kufungua rasmi kesi ya talaka baada ya ndoa yao kudumu kwa miaka 29.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa mahakamani, Tomeka anadai euro milioni 100 kama sehemu ya mgawanyo wa mali, akisema kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga utajiri na mafanikio ya Akon tangu mwanzo wa safari yake ya muziki.
Hata hivyo, ripoti ya awali ya ukaguzi wa mali iliyowasilishwa mahakamani imeibua mshangao baada ya kubaini kuwa Akon ana kiasi cha dola 10,000 pekee kwenye akaunti yake binafsi, huku mali na fedha nyingine zikidaiwa kuwekwa kwa jina la mama yake.
Kesi hiyo sasa imezua gumzo kubwa mitandaoni, huku mashabiki na wadau wa muziki wakitilia shaka taarifa hizo za kifedha, wakijiuliza ikiwa msanii huyo ambaye amekuwa akihusishwa na miradi mikubwa ya maendeleo barani Afrika, hasa mradi wa “Akon City” nchini Senegal, kweli amefikia hatua ya kifedha ya namna hiyo.
Mahakama inatarajiwa kusikiliza ushahidi zaidi katika wiki zijazo ili kubaini ukweli wa madai hayo na kupanga namna ya kugawa mali kati ya wawili hao.