Msanii nyota wa Bongo Fleva Nandy amekanusha madai ya kuishi maisha ya kuigiza mtandaoni, akisema kuwa anachokionesha kwenye mitandao ya kijamii ni uhalisia wa maisha yake.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye Snapchat, Nandy amesema amekuwa akipokea jumbe kutoka kwa baadhi ya watu wanaodai kuwa mafanikio anayoyaonesha, ikiwemo magari na maisha ya kifahari, si ya kweli. Amesema kuwa hana sababu ya kuigiza maisha ili kuwafurahisha watu, kwani anachofurahia ni matokeo ya juhudi zake binafsi.
Msanii huyo amefafanua kuwa ameshapita hatua ya kufanya mambo kwa ajili ya kutafuta sifa, akiongeza kuwa kila anachoposti ni sehemu ya maisha yake halisi. Amesema pia kuwa kwa muda mrefu amekuwa akipuuza maneno ya wakosoaji, lakini ameamua kunyosha maelezo ili kuondoa sintofahamu.
Kauli ya Nandy inakuja baada ya baadhi ya mashabiki kutilia shaka gari aina ya G-Wagon ambalo inadaiwa alijinunulia kama zawadi ya Siku ya Wapendanao. Wapo waliodai huenda gari hilo si mali yake bali ni la kukodi kwa ajili ya kupiga picha na kujiongezea hadhi mtandaoni.