Mchekeshaji na mwanaharakati wa kijamii Eric Omondi ameanza rasmi ujenzi wa taasisi ya Sisi Kwa Sisi Rescue baada ya kukamilisha safari ya kutembea kwa miguu kutoka Nairobi hadi Mombasa kwa ajili ya kuchangisha fedha.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Eric amethibitisha kuwa ndoto hiyo sasa imeanza kutimia, akieleza kuwa tayari wameweka jiwe la msingi kwenye ardhi waliyonunua ili kuanza ujenzi wa kituo hicho. Amesema kuwa timu yake iko kazini kwa sasa kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Mradi huo unalenga kujenga kituo cha uokoaji (rescue centre), shule ya sekondari ya bure, ghala la kuhifadhi misaada pamoja na ununuzi wa ambulensi ili kusaidia familia zenye uhitaji katika jamii.
Hatua hiyo imepokelewa kwa hisia mseto huku wengi wakimpongeza kwa juhudi zake za kusaidia jamii, hasa baada ya safari yake ndefu ya kutembea mamia ya kilomita kama njia ya kuhamasisha umma kuchangia mradi huo.