Director Trevor Ampongeza Bien kwa Kumlipa Vizuri GenZ Goliath Katika Video Mpya ya Muziki
Mkurugenzi Mkuu wa Watayarishaji wa Maudhui ya Kidijitali nchini Kenya, Director Trevor, amemsifu msanii Bien kwa kumuonesha heshima ya hali ya juu Gen Z Goliath kwa kumlipa vizuri na kumhudumia ipasavyo kwa ajili ya kuonekana kwa muda mfupi kwenye video ya muziki. Kupitia mitandao ya kijamii, Director Trevor ameweka wazi kuwa Bien alifuata taratibu zote za kazi kwa kulipa kiwango kamili cha malipo, kugharamia usafiri wa Goliath kwa kutumia gari la kifahari aina ya Toyota LX570, pamoja na malazi ya kiwango cha juu wakati wa kutayarisha video ya wimbo wake mpya “All My Enemies Are Suffering” Hii ni tofauti na matukio ya awali ambapo wasanii na waigizaji chipukizi walilalamika kutolipwa au kupuuzwa baada ya kuchangia mafanikio ya kazi mbalimbali za burudani. Mashabiki wengi wamelipongeza tukio hilo wakisema kuwa ni mfano wa kuigwa kwa wasanii wakubwa kuonyesha heshima na kuthamini mchango wa vipaji vinavyochipuka. Aidha, hatua hiyo imeibua matumaini kwa vijana wengi kuwa na imani na kazi yao huku wakijua kuwa juhudi zao zinaweza kutambuliwa na kuthaminiwa kikamilifu. Video ya wimbo mpya wa Bien,“All My Enemies Are Suffering” umewavutia wengi si tu kwa ubora wa maudhui bali pia kwa jinsi ulivyowajumuisha majina maarufu kama DJ Shiti na Gen Z Goliath, ambao wameongeza ucheshi na mvuto katika video hiyo.
Read More