Diamond Platnumz Apokea Tuzo ya Diamond Play Button Kutoka YouTube
Msanii nyota wa muziki wa Bongo Flava, Diamond Platnumz, ameweka rekodi mpya baada ya kukabidhiwa tuzo ya kifahari ya Diamond Play Button kutoka YouTube, ikiwa ni kutambua mafanikio ya kufikisha zaidi ya wafuasi milioni 10 kwenye chaneli yake rasmi. Tukio hilo lilifanyika jijini New York, Marekani, na linamweka Diamond katika nafasi ya kipekee kama mmoja wa wasanii wachache kutoka Afrika kufikia kiwango hicho. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond alithibitisha kupokea tuzo hiyo huku akionyesha shukrani kwa mashabiki, timu yake, familia, na YouTube kwa mafanikio hayo makubwa. “Thank you YouTube, My Fans, Team & Family! 10+ Million YouTube Subscribers 🙏🏽🔥” Aliandika Instagram. Diamond anakuwa msanii wa nne kutoka Afrika kupokea Diamond Play Button, akiungana na wasanii kama Mohamed Ramadan, Saad Lamjarred, na Soolking. Tuzo hii hutolewa na YouTube kwa chaneli zilizofikisha au kupita subscribers milioni 10, na ni alama ya ushawishi mkubwa wa kidijitali duniani. Mafanikio haya yanaimarisha nafasi ya Diamond si tu kama msanii wa Tanzania au Afrika Mashariki, bali pia kama nembo ya muziki wa Afrika kwenye majukwaa ya kimataifa. Mashabiki wake wamekuwa nguzo muhimu katika safari yake ya muziki, wakichangia kwa namna ya kipekee kwa kuangalia, kushirikisha na kusambaza kazi zake mtandaoni kwa zaidi ya muongo mmoja.
Read More