Lydia Jazmine Amshauri Spice Diana Aache Kumzungumzia Roger Lubega Hadhrani
Msanii wa muziki kutoka Uganda, Lydia Jazmine, amemshauri Spice Diana kujiepusha na mazungumzo ya mara kwa mara kuhusu aliyekuwa meneja wake Roger Lubega kwenye vyombo vya habari, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri safari yake ya muziki. Akizungumzia suala hilo, Lydia Jazmine amesema kuwa Diana akiendelea kumzungumzia meneja wake wa zamani kutazua mijadala isiyo ya lazima miongoni mwa mashabiki na wadau wa tasnia ya burudani. Kwa mujibu wake, mjadala huo unaweza kumkwamisha Spice Diana katika jitihada zake za kusonga mbele na kuendelea kukuza kazi yake ya muziki. Msanii huyo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Spice Diana kuelekeza nguvu zake katika muziki na mipango mipya badala ya kurejelea masuala yaliyopita. Amesema kuwa ukimya na nidhamu ya mawasiliano vinaweza kumsaidia msanii yeyote kulinda taswira yake na kudumisha mwelekeo chanya wa kazi yake. Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Spice Diana alitangaza kuachana na meneja wake wa muda mrefu Roger Lubega, jambo lililozua mjadala kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ikizingatiwa kuwa wawili hao waliwahi kudaiwa ni wapenzi.
Read More