Mke wa mwanamitindo wa mavazi Bolo Bespoke, anayejulikana kama Mueni, amezua gumzo mtandaoni baada ya kuweka wazi matakwa yake ya baada ya kifo, akisisitiza kuwa hataki kupakwa makeup wala kuvishwa wig wakati wa mazishi yake.
Kupitia video aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa TikTok, Mueni ameeleza kuwa hajawahi kupenda kupaka makeup wala kuvaa wig, akisisitiza kuwa anatamani kuzikwa katika hali yake ya asili.
Mrembo huyo amesema kuwa licha ya kuvaa makeup mara chache kutokana na majukumu ya kazi, si jambo analolipenda. Ameongeza kuwa angepata nafasi kuchagua maisha anayotamani kuishi, angependelea kunyoa nywele zake na kubaki katika sura yake ya kawaida bila makeup, ili ngozi yake ipumue na aendelee kuishi kwa uhuru anaoupenda.
Kauli hiyo ya Mueni imeibuka siku chache baada ya wosia unaodaiwa kuwa wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kusambaa mtandaoni, ambapo alielekeza kuwa azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake, jambo lililochochea mjadala mpana kuhusu matakwa ya watu binafsi wakati wa mazishi.