Mchekeshaji na mwanaharakati wa masuala ya kijamii Eric Omondi amefanikiwa kukamilisha safari yake ya kutembea kwa miguu kutoka Nairobi hadi Busia ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuchangisha fedha za kujenga kituo cha uokoaji kupitia mpango wake wa Sisi Kwa Sisi.
Kupitia ujumbe alioutuma baada ya kukamilisha safari hiyo, Eric amesema hatua hiyo ilikuwa zaidi ya juhudi zake binafsi, bali ilikuwa ni ishara ya mshikamano wa Wakenya kusaidiana.
Omondi ametoa shukrani kwa kila mtu aliyeshiriki katika safari hiyo kwa njia mbalimbali, ikiwemo kutembea naye, kutoa michango, kusambaza ujumbe wa kampeni na kuunga mkono mradi huo tangu mwanzo hadi mwisho.
Kupitia kampeni ya Sisi Kwa Sisi, Eric Omondi amekuwa akihamasisha Wakenya kusaidiana badala ya kusubiri msaada kutoka nje, huku mradi wa kituo cha uokoaji ukitarajiwa kusaidia watu wenye mahitaji maalum na wale wanaohitaji msaada wa haraka katika jamii.