Msanii wa muziki wa Bongo Fleva Barnaba Classic amefunguka kuhusu changamoto alizopitia mwanzoni mwa safari yake ya muziki, akisema aliwahi kulala studio na kufanya kazi mbalimbali ikiwemo usafi hadi kupika alipokuwa chini ya taasisi ya kukuza vipaji ya Tanzania House of Talent (THT).
Barnaba amesema kipindi hicho alikuwa chini ya uongozi wa marehemu Ruge Mutahaba na alilazimika kuvumilia hali hiyo kwa sababu alikuwa na ndoto ya kufanikiwa katika muziki. Kwa mujibu wake, licha ya changamoto na tofauti ndogo ndogo zilizowahi kujitokeza, bado anaona hakuna sababu ya kuwasema vibaya watu waliomsaidia katika safari yake.
Aidha, Barnaba amewataka watu wanaosaidia vipaji chipukizi kuhakikisha wanawatendea vijana hao kwa wema wanapowasaidia kufikia ndoto zao, ili hata wakiondoka baadaye waweze kuwakumbuka kwa mema.
Kauli ya Barnaba imeibuka wakati sakata linaloendelea mitandaoni likihusisha msanii Mac Voice, ambaye hivi karibuni alidai kuwa aliwahi kulala studio alipokuwa akijaribu kupambana kufikia mafanikio katika muziki. Kauli hiyo imezua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya wasanii wakisimulia changamoto walizokumbana nazo mwanzoni mwa safari zao za muziki.