Msanii nguli wa muziki kutoka Uganda, Jose Chameleone, ameadhimisha mwaka mmoja tangu alipougua na kulazwa kwa muda mrefu, tukio ambalo liliwagusa mashabiki na wadau wengi wa muziki Afrika Mashariki.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Chameleone amesema kuwa siku kama ya leo mwaka mmoja uliopita alikuwa amelazwa kitandani akipambania maisha yake. Ameeleza kuwa kipindi hicho kilikuwa kigumu, lakini kilibadilika kuwa cha matumaini kutokana na msaada mkubwa alioupata kutoka kwa familia, marafiki na mashabiki.
Msanii huyo ameeleza kuwa maombi, ujumbe wa faraja, simu pamoja na ziara kutoka kwa watu mbalimbali vilimpa nguvu na matumaini yaliyomsaidia kuvuka kipindi hicho kigumu.
Chameleone amesema kuwa bila mchango wa wadau wote, asingefikia hatua alipo sasa kiafya. Amehitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia wote Krismasi njema na heri ya Mwaka Mpya, huku akisisitiza kuwa anathamini sana upendo na mshikamano alioupata kutoka kwa mashabiki wake.