Msanii wa muziki kutoka Kenya, Mr Seed, amewataka watu kuwa makini na kumuomba Mungu kwa bidii zaidi katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka, akieleza kuwa vifo na ajali vimeongezeka kwa kiwango cha kutisha.
Kupitia ujumbe aliouchapisha mitandaoni, Mr Seed amesema ndani ya dakika chache tu baada ya kuingia mtandaoni, alikutana na taarifa nyingi za watu kupoteza maisha, hususan kutokana na ajali za barabarani. Ameeleza kuwa hali hiyo inatia hofu kubwa, hasa wakati huu ambao wengi wanasafiri mikoani na kusherehekea mwisho wa mwaka.
Msanii huyo amegusia pia tukio la kusikitisha la mtoto aliyefariki katika eneo la Pipeline jijini Nairobi baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya saba, tukio lililoibua huzuni na maswali mengi miongoni mwa wananchi.
Kwa mtazamo wake wa kiimani, Mr Seed amesisitiza kuwa kuna haja ya watu kusimama pamoja katika maombi, akisema kipindi hiki kinahitaji uangalizi wa kiroho na tahadhari zaidi. Amewahimiza watu kuomba kwa ajili yao wenyewe, marafiki na familia zao ili kupata ulinzi na faraja.