Rapa kutoka Kenya, Khaligraph Jones, ametangaza rasmi kuingia kwenye mchezo wa masumbwi, hatua inayoongeza sura mpya katika mjadala wa wasanii wanaojitosa kwenye michezo ya ushindani.
Kupitia Instastory yake, Khaligraph ameeleza kuwa anatafuta kocha wa ngumi atakayemsaidia kujiandaa kwa mapambano maalum dhidi ya wasanii wengine mwaka 2026. Ingawa hakutaja majina ya wapinzani anaowalenga, ujumbe wake umeibua gumzo miongoni mwa mashabiki na wadau wa burudani na michezo.
Khaligraph, ambaye mara kwa mara ameonekana akifanya mazoezi ya nguvu na kujihusisha na mafunzo ya mwili, amekuwa akijielekeza zaidi kwenye shughuli za mazoezi katika miezi ya hivi karibuni, na hatua hii imeonekana kama mwendelezo wa kujitanua nje ya muziki.
Kwa sasa, mashabiki wanasubiri updates zaidi kuhusu kocha atakayemsimamia na tarehe rasmi za mazoezi na mapambano yajayo.