Mwigizaji nyota wa filamu za Bongo, Wastara Juma, amewatolea uvivu watu wanaoponda na kudharau uhusiano wake na mwanamuziki mkongwe wa Bongo Flava, Dudu Baya.
Akiwa amechoshwa na maneno ya kashfa, Wastara ameapa kulilinda penzi hilo kwa nguvu zake zote, akisisitiza kuwa Dudu Baya ni mwanaume kama walivyo wanaume wengine na ana haki ya kupendwa na kupewa heshima.
Aidha, amekemea vikali dhana inayozungumzwa na wengi kuwa wanaume kutoka kabila la Wasukuma ni wakatili, akisema yeye hatasikiliza maneno ya mtandaoni wala majungu ya watu.
Tangu Wastara Juma, na mwanamuziki mkongwe wa Bongo Flava, Dudu Baya (Konki), watangaze rasmi uchumba wao, mitandao ya kijamii imelipuka kwa hisia mseto, huku mashabiki wengi wakipinga vikali hatua hiyo.
Hoja kubwa ya mashabiki imekuwa ni sifa ya ukorofi inayomandama Dudu Baya kwa miaka mingi, ambapo wengi wameelezea hofu yao kuwa huenda Wastara akaishia kudhalilishwa au kuumizwa kutokana na tabia za msanii huyo anayejulikana kwa msimamo mkali.