Streamer na YouTuber maarufu duniani, IShowSpeed, amepigwa na butwaa baada ya kukutana ana kwa ana na kijana Gen Z Goliath, anayesemekana kuwa kijana mrefu zaidi nchini Kenya kwa kimo.
Kupitia YouTube Live, IShowSpeed ameonekana akishindwa kuficha mshangao wake alipomuona kijana huyo, huku akimkazia macho kwa muda kabla ya kumuuliza ikiwa ndiye mtu mrefu zaidi barani Afrika.
Kilichozidi kumshangaza zaidi IShowSpeed ni ukubwa wa kiatu cha Gen Z Goliath, jambo lililomfanya aonyeshe mshangao mkubwa na kuendelea kumtazama kwa makini, kana kwamba haamini macho yake.
Katika mazungumzo yao, Speed alionekana kuvutiwa sana na maumbile ya kijana huyo, akimsifia na kusema hajawahi kukutana na mtu wa kimo kama hicho.
Kukutana kwa wawili hao kumezua gumzo kubwa mitandaoni, na wengi wakimpongeza Gen Z Goliath kwa kuibeba Kenya kwenye ramani ya dunia, huku wakimshukuru IShowSpeed kwa kuonyesha upekee na vipaji vinavyopatikana barani Afrika.