Mwanamitandao kutoka nchini Tanzania, Kiredio, amedai kuwa watengeneza maudhui (content creators) wanaingiza kipato kikubwa zaidi kuliko wasanii wengi wa muziki wa Bongofleva wanaofahamika na kushangiliwa mitaani.
Kupitia InstaStory yake, Kiredio ameposti moja ya mikataba yake ya kazi ikionesha analipwa kiasi cha shilingi milioni 17 kwa kazi moja tu na kusisitiza kuwa sekta ya utengenezaji maudhui ina fedha nyingi, lakini mara nyingi taarifa za mikataba na malipo hubaki kuwa siri.
Aidha, amewataka watu kuacha kuwachukulia poa watengeneza maudhui na badala yake kuwapa heshima wanayostahili kwani sekta hiyo ina fedha nyingi kwa wanaoweka juhudi na ubunifu wa hali ya juu.
Kauli yake imezua mjadala mpana mtandaoni, huku baadhi ya watu wakikubaliana naye kwamba tasnia ya maudhui ya kidijitali imekua kwa kasi na inalipa, na wengine wakibaki na maswali kuhusu uwiano wa mapato kati ya wanamuziki na watengeneza maudhui.