Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Nay wa Mitego, amesema hatua ya baadhi ya mashabiki kuonyesha kutoridhishwa na wasanii wa Tanzania ni somo muhimu ambalo linapaswa kuwafanya wasanii kurejea kwenye misingi ya kuwaheshimu na kuwasikiliza wananchi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nay wa Mitego ameeleza kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiwashauri wasanii wenzake kujitokeza na kusimama na wananchi angalau mara moja kwa mwaka, kwa sababu mashabiki ndio mabosi wao wa kwanza na ndio wenye nguvu ya kuamua thamani na ushawishi wa msanii.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Nay amesema kuwa mara nyingi ametoa mifano ya wasanii kutoka nje ya Tanzania pamoja na katika nchi jirani ambao huonyesha mshikamano na jamii yao pindi linapotokea jambo linalowahusu wananchi.
Msanii huyo, amesema changamoto kubwa kwa baadhi ya mastaa wa Tanzania ni ubinafsi na kusahau kuwa nguvu na mafanikio yao yanatokana na wananchi wanaowaunga mkono. Kwa sasa, ameongeza kuwa mashabiki wameamua kuonyesha wazi uthibitisho kwamba wao ndio wanaowapa wasanii jeuri na maisha mazuri kupitia sapoti yao.
Nay wa Mitego amesisitiza kuwa haoni kosa kwa Watanzania kuendelea na msimamo waliouchukua hadi hasira zao zitakapopungua. Anaamini kuwa hali hii itageuka kuwa funzo muhimu litakalowaunganisha wasanii na wananchi, na kuleta lugha moja ya ushirikiano na kuheshimiana katika tasnia ya burudani nchini Tanzania